WANAWAKE WAJASIRIAMALI MASASI WAHAMASISHWA KURASIMISHA BIASHARA

 

Bw. Suleiman Suleiman (aliyesimama kushoto)akitoa elimu kwa washiriki wa Semina ya wajasiriamali wanawake Halmashauri ya wilaya ya Masasi.

Mbunge wa Viti Maalum(UWT) mkoa wa Mtwara Mhe. Agnes Hokororo akiwa katika picha ya pamoja na wakufunzi na baadhi ya washiriki wa semina kuhusu huduma zinazotolewa na Wakala wa Usajili wa Biashara na Leaeni (BRELA) iliyofanyika wilayani Masasi

Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) imewataka wanawake wajasiriamali wa Halmashauri ya wilaya ya Masasi kusajili kampuni na majina ya biashara ili biashara zao zitambulike kisheria.

Rai hiyo imetolewa na Msaidizi wa Usaijili wa BRELA Bw. Suleiman Suleiman wakati akitoa elimu kwa wanawake wajasiriamali 110 kutoka Halmashauri ya wilaya ya Masasi iliyofanyika tarehe 29 Aprili, 2023 wilayani humo.

Bw. Suleiman amesema pamoja na changamoto wanayokumbana nayo wajasiriamali wengi katika kutumia mfumo wa Usajili kwa Njia ya Mtandao, BRELA iko tayari wakati wote kutoa usaidizi hivyo wanapokwama wasisite kuwasiliana na BRELA kupitia kituo cha miito ya simu ili kupatiwa usaidizi.

Bw. Suleiman amesema BRELA imekuwa ikitoa elimu kwa wadau mbalimbali wakiwemo wajasiriamali ili kuhakikisha kuwa wadau wote wananufaika kutokana na sajili pamoja na leseni zinazotolewa na BRELA.

"Kuna manufaa mengi ambayo mnaweze kupata kutokana na kurasimisha biashara zenu kwani mbali na kulindwa kisheria pia kuna fursa za kupata mikopo kutoka taasisi za kifedha pamoja kupata zabuni mbalimbali serikalini", anafafanua Bw. Suleiman.

Kwa upande wake Msadizi wa Usajili wa BRELA Bw. Athuman Makuka amewaelimisha wanawake hao umuhimu wa kuwa na alama za biashara katika bidhaa zao ili ziweze kutambulika.

Amesema watakaposajili alama za biashara itakuwa rahisi kwa bidhaa zao kujitofautisha na nyingine, hivyo kuwa na uhakika na soko la bidhaa zao. Usajili pia utamuwezesha mjasiriamali kupata haki ya kipekee ya alama ya biashara au huduma ambayo itasaidia kuzuia wengine kutumia alama yake sokoni ili kujipatia manufaa kinyume na sheria lakini pia itamuwezesha mjasiriamali kuhimili soko la ushindani kwakuwa itakuwa ni rahisi wateja kutambua bidhaa yake sokoni.

Naye Afisa Leseni wa BRELA Bw. Jubilate Muro amewasihi wajasiriamali kusajili viwanda vidogo BRELA kwani katika wilaya hiyo wengi wao wana viwanda vidogo vya kubangua korosho, kutengeneza sabuni na batiki ambavyo kisheria vinapaswa kusajiliwa.

Awali akifungua mafunzo hayo Mbunge wa Viti Maalum(UWT) mkoa wa Mtwara Mhe. Agnes Hokororo ameshukuru jitihada zinazofanywa na BRELA kuwafikia wadau mahali walipo na kuwapatia elimu.

Mhe. Hokororo amesema kwakuwa wanawake wengi wilayani humo wamejikita katika sekta isiyo rasmi ili waweze kujikomboa kiuchumi, mafunzo haya yamefika wakati muafaka kwani watanufaika na kuwa mabalozi wa kufikisha elimu ya BRELA kwa wengine.

Mhe. Hokororo amekiri kuwa wajasiriamali wengi wilayani humo hawajasajili majina ya biashara hivyo elimu ya BRELA itawawezesha kufuata utaratibu wa kusajili majina ya biashara.

Wanawake wajasiriamali wa Halmashauri hiyo wamepatiwa elimu kuhusu Usajili wa Majina ya Biashara na Kampuni, Alama za Biashara na Huduma na jinsi ya kupata leseni za biashara na viwanda.

Semina hiyo ya siku moja iliratibiwa na Halmashauri ya wilaya ya Masasi.  

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments