MANISPAA YA SHINYANGA YAIBUKA MSHINDI WA JUMLA MAADHIMISHO SIKU YA WAFANYAKAZI MEIMOSI

 


Na Shinyanga MC.

Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga imeibuka kuwa mshindi wa jumla kwa kutoa zawadi kwa wafanyakazi wake hodari katika Maadhimisho ya Sherehe ya Siku ya Wafanyakazi Duniani (MEI MOSI) kwa Mkoa wa Shinyanga ambapo imetoa zaidi ya milioni 30 kwa mwaka huu wa 2023.

Pongezi hizo zimetolewa leo tarehe 1 Mei, 2023 na Mhe. Christina Solomon Mndeme Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga wakati akikabidhi zawadi mbalimbali kwa wafanyakazi ambao wamechaguliwa kutoka Taasisi zao hafla ambayo imefanyika katika Uwanja wa Mwadui uliopo Wilaya ya Kishapu.

Mhe. Mndeme ambaye alikuwa Mgeni Rasmi katika Maadhimisho hayo, pamoja na kueleza mazuri yaliyofanywa na Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, lakini pia amewakumbusha watumishi juu ya wajibu wao katika uwajibikaji wa kweli kwenye majukumu yao ili kuiletea maendeleo Serikali yetu.

Aidha amewakumbusha juu ya kulinda Maadili ya kitanzania, ambapo amewaeleza kuwa Tanzania kama Nchi tuna maadili na tamaduni zetu tulizorithi kutoka kwa mababu zetu na viongozi wetu huku akiwataarifu kuwa Mkoa wa Shinyanga umeanzisha Kampeni ijulikanayo kama DON'T TOUCH ME, HAPA NI KWANGU ambayo inalenga kuwaelimisha watu wote na kwamba elimu hii iende mpaka kwa familia.

" Wakati tunasherehekea Maadhimisho haya, pamoja na kuipongeza sana Serikali yetu lakini tujiandae kuipokea Kampeni hii ambapo itakwenda mpaka ngazi ya familia ambapo tuwafundishe watoto na tunaowalea kukataa kabisa tabia zote zisizokuwa na maadili na wawe tayari kusema DON'T TOUCH ME, HAPA NI KWANGU pia mkumbuke uwajibikaji na maadili yetu pamoja na kuthamini Ulinzi na Usalama ambapo wenyeviti wetu wasiruhusu mtu kuingia maeneo yao kama hajulikani na ikitotea watoe taarifa kwa Mamlaka za Usalama," alisema Mhe. Mndeme.

Maadhimisho ya Mei Mosi 2023 Kimkoa yamefanyika katika Uwanja wa Mwadui, Wilaya ya Kishapu yakiwa na KAULI MBIU: Mishahara Bora na Ajira za Staha, Ni Nguzo kwa Maendeleo ya Wafanyakazi. Wakati ni Sasa!

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments