WAZIRI MHAGAMA,SIMBACHAWENE WAKABIDHIANA OFISI

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Jenista Mhagama akizungumza na Watumishi wa Ofisi hiyo (hawapo pichani)  wakati wa makabidhiano ya Ofisi kati yake na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi  wa Umma na Utawala Bora Mhe. George Simbachawene yaliyofanyika Jijini Dodoma..

Aliyekuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. George Simbachawene  ambaye kwa sasa ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi  wa Umma na Utawala Bora akimkabidhi nyaraka  Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu)  Mhe. Jenista Mhagama  wakati wa hafla ya  makabidhiano ya Ofisi  kati yao.  Kulia ni Katibu  Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Dkt. Jim Yonazi katika Ukumbi wa Ofisi hiyo  Aprili 06, 2023 Jijini Dodoma.


Na Mwandishi wetu, DODOMA.


WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Jenista Mhagama amewataka watumishi wa umma kutekeleza  majukumu yao ipasavyo  kwa ajili ya maendeleo ya wananchi na Taifa kwa ujumla.

Ameyasema hayo wakati wa hafla ya makabidhiano  kati ya aliyekuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Mhe. George Simbachawene na aliyekuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Jenista Mhagama mara baada ya uteuzi uliyofanywa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia  Suluhu Hassan  Aprili 01 mwaka 2023.

Waziri  Mhagama  amesema dhamira ya mtumishi wa umma Nchini ni kuhakikisha anatimiza wajibu wake kikamilifu katika kuwahudumia wananchi mahali na kwa nafasi yoyote anayopangwa  kwa kuzingatia miongozo na taratibu  zilizopo.

“Mara zote dhamira ya mtumishi wa umma  Nchini ni kuhakikisha kila unapopangwa unafanya kazi kwa nguvu zako zote pamoja na utii  na kuwa tayari kutumikia Taifa mahali popote kwahiyo kurudi kwangu hapa najihesabu ni sehemu yenu pia kama mtumishi wa umma,” Amesema Mhe. Jenista.

Pia amebainisha kwamba Ofisi ya Waziri Mkuu ambayo ina jukumu la kuratibu shughuli za Serikali haiwezi kufanikiwa ikiwa watumishi wake watashindwa kujidhatiti na kufanya kazi kwa moyo kwa kuzingatia mazingira husika.

“Msingi wa tija katika utendaji wa kazi Serikalini  unatutaka  kuwa na uratibu mzuri unaozingatia sera, miongozo na kanuni zilizopo kwa kuzingatia jukumu kubwa la Ofisi ya Waziri Mkuu ni kuratibu shughuli zote za Serikali na tuna jukumu la kusimamia Bunge kama mhimili mwingine ndani ya Nchi hivyo bila kuwa na ushirikiano hatutafikia malengo tunayokusudia,” Ameeleza.

Kwa upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. George Simbachawene amemshukuru  Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa  kumuamini na kumpa  fursa ya kulitumikia Taifa pamoja na watumishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu  kwa ushirikiano wakati wote wa utekelezaji wa majukumu yake.

“Nitumie nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kuniamini  kuendelea  kuwatumikia wananchi katika nafasi hii na watumishi pia nawashukuru kwa ushirikiano mlionipatia na kuwezesha kufanikisha shughuli za uratibu kwa kipindi chote,” Ameshukuru Mhe. Simbachawene.

Naye Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Dkt. Jim Yonazi amemshukuru Mhe. Simbachawene kwa utumishi wake mwema katika Ofisi hiyo.

Aidha ametumia nafasi hiyo kumkaribisha Mhe. Waziri Mhagama katika Ofisi ya Waziri Mkuu na kuahidi kumpa ushirikiano ili kufikia malengo ya Serikali ya kuwatumikia wananachi.

 

 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post