WANNE WAFA KWA TUHUMA ZA WIZI WA KUTUMIA SILAHA




Na Dotto Kwilasa , Dodoma.


Jeshi la Polisi Mkoani hapa limewathibiti majambazi wanne wa kiume ambao majina yao bado hayajatambulika wenye umri kati ya 25-30 waliokuwa katika harakati za kufanya tukio la unyang'anyi wa kutumia silaha nyumbani kwa  Edna Joseph Kashashari (41), mfanyabiashara.

Kwa mujibu wa  Kamanda wa Jeshi la polisi Dodoma Martine Otieno tukio hilo limetokea Aprili 25,2023 majira ya saa 03:10 usiku mtaa wa Mwangaza, Kisasa Kata ya Dodoma Makulu.

Akizungumza na Waandishi wa habari leo Aprili 26,2023 Kamanda Otieno amesema majambazi hao walivamia nyumbani kwa Bi. Edna Joseph Kashashari (41), mfanyabiashara, mkazi wa Kisasa wakiwa wamevaa barakoa usoni na kufanikiwa kunyang'anya pesa taslim 1,100,000/= simu ya Samsung moja na simu ndogo tatu baada ya watu hao kumtishia kumkata mapanga ndipo mhanga alipiga kelele za kuomba msaada.

“Baada ya mhanga kupiga kelele za kuomba msaada  zilisikika kwa majirani ambapo majirani hao walitoa taarifa kwa askari  waliokuwa doria eneo hilo ambao walifika kwa haraka na kuwakuta watu hao ambao walijihami kwa kutaka kuwashambulia askari kwa mapanga na askari hao kujibu mapigo kwa kuwafyatulia risasi ambazo ziliwajeruhi watuhumiwa hao maeneo mbalimbali ya miili yao,”amesema.

Ameongeza kuwa majambazi hao walijificha nyuma ya ukuta wa fensi na kuruka ukuta huo na kwenda kumvizia Edna Joseph Kashashari wakati anataka kufunga mlango wa nyumba na kumtishia kumkata na mapanga kisha kumpora vitu hivyo.

Hata hivyo amesema watu hao wamefariki dunia wakiwa wanapelekwa hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Dodoma kwa matibabu.

“Wamepata walichostahili,hiyo ndiyo adhabu yao,Kwa yeyote ambaye hajamuona ndugu yake anaweza kwenda hospitali ya Rufaa ya Mkoa kuona miili hiyo kubaini kama ni ndugu yake,"amesisitiza 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments