TANZANIA NA UJERUMANI ZAWEKA MIKAKATI KABAMBE KUPUNGUZA MIGOGORO BAINA YA WANYAMAPORI NA BINADAMU


👉 Ujerumani yatoa bilioni 16

Na John Mapepele

SERIKALI ya Ujerumani kupitia Shirika lake la Maendeleo la Kimataifa (GIZ) imetoa msaada wa Euro milioni 6 (16 bilioni) kusaidia juhudi za serikali katika uhifadhi wa bioanuai na kukabiliana na Migogoro ya Wanyamapori (HWC) na binadamu kwenye Maeneo ya Hifadhi.

Tukio hilo la kihistoria limeshuhudiwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mohammed Mchengerwa na Balozi wa Ujerumani nchini, Regine Hess, na wadau mbalimbali wa uhifadhi leo jijini Dar es Salaam, ambapo mkataba huo umesainiwa na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Hassan Abbasi kwa upande wa Tanzania na Dkt. Mike Falke, Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Ujerumani (GIZ).




Aidha, Mhe. Mchengerwa amefafanua kuwa pamoja na mambo mengine lengo la fedha hizo ni Kupambana na Wanyama Waharibifu katika maeneo ya Kusini ya Kusini mwa Tanzania ambapo ameiomba Serikali ya Ujerumani kuendelea kunisaidia Tanzania kwenye uhifadhi wa raslimali.

Waziri Mchengerwa ameongeza kuwa mradi huo wa miaka mitatu utakaotekelezwa katika mfumo ikolojia wa Selous kusini mwa Tanzania, mbali na kukabiliana na HWC utasaidia katika kulipa fidia kwa jamii zilizoathirika na wanyama.

Mhe. Mchengerwa amebainisha kuwa jamii zitawezeshwa kupitia mafunzo ya mbinu sahihi za kukabiliana na hali hiyo pamoja na kurahisisha matumizi ya teknolojia za kisasa katika kupunguza HWC kama vile kupaka rangi za tembo na uzio wa kijiografia.

Amesema Serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali za kuimarisha shughuli za uhifadhi ambazo ni pamoja na kuandaa Mkakati wa Kitaifa wa Usimamizi wa HWC-2020/2024.

Amesema kupitia mkakati huo, wizara imeanzisha vituo 154 vya Askari wa uhifadhi nchini kote ili kukabiliana na HWC, na kuongeza vituo vingine 15 vitajengwa kabla ya mwisho wa Juni 2023.

Amesema zaidi ya skauti 180 ngazi ya vijiji (VGS) wamepatiwa mafunzo na kuwezeshwa kukabiliana na HWC, akibainisha kundi jingine la VGS 120 litaanza mafunzo mwishoni mwa mwezi huu.

Ameongeza: “Katika kushughulikia HWC, serikali inafanya kazi na washirika wa uhifadhi na maendeleo katika kujenga uwezo wa taasisi na jumuiya zake.

Mhe. Mchengerwa ameeleza kuwa Serikali ya Ujerumani ni mdau mkubwa katika uhifadhi wa bioanuwai ambapo amekuwa na mchango mkubwa katika suala la uhifadhi kwa zaidi ya miaka 60.”

Kwa miaka sita iliyopita, Serikali ya Ujerumani imesaidia shughuli za uhifadhi kupitia ruzuku zenye thamani ya Euro milioni 124, alisema.

Regine Hess, Balozi wa Ujerumani nchini amepongeza Tanzania katika suala la uhifadhi huku akisisitiza kuwa Tanzania imeweza kuhifadhi sehemu kubwa ya ardhi yake ikilinganishwa na mataifa mengine mengi.




Amesema juhudi za uhifadhi zimesababisha ongezeko la wanyamapori wakiwemo tembo.

“Idadi ya wanyama imeongezeka; lakini kupitia uhifadhi pia tunaimarisha utalii na kutengeneza ajira,” alisema Hess.

Amesema Serikali yake inaunga mkono juhudi za uhifadhi wa bioanuwai na kupunguza HWC kwa sababu wakati mwingine migogoro husababisha watu kuuawa.

Aidha, amefafanua kuwa Serikali yake pia iko tayari kuisaidia Tanzania katika kuandaa Mkakati wa Kitaifa wa Utalii ili kuboresha utalii nchini.

Dkt. Mike Falke, Mkurugenzi wa GIZ nchini Tanzania na Jumuiya ya Afrika Mashariki alisema wamekuwa wakitoa msaada katika kukabiliana na HWC pamoja na sekta nyinginezo kama vile maji, afya, kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi na Unyanyasaji wa Kijinsia (GBV), miongoni mwa mengine.

Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Maurus Msuha amesema kupitia mradi huo jamii zinatarajiwa kunufaika kupitia Maeneo ya Hifadhi ya Wanyamapori (WMAs).

“Uhifadhi ni kwa ajili ya watu; inachangia ukuaji wa uchumi na maendeleo ya watu,” alisema Dkt. Msuha.




Sekta ya utalii inatoa ajira kwa watu milioni 1.5 kote nchini.

“Kusainiwa kwa mkataba huu ni ishawa kuwa Serikali imeanza na itaendelea kulipa uzito suala la uhufadhi na hasa kupunguza athari za wanyama waharibifu kama tembo kwa kushirikiana na wadau kama mnavyoona hapa leo,” alisema Waziri Mchengerwa.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post