PURA, EACOP WABADILISHANA UZOEFU USHIRIKI WA WATANZANIA

Meneja wa Ushiriki wa Wazawa wa Kampuni ya EACOP, Bw. Olivier Foulonneau (wa kwanza kushoto), Mkuu wa Masuala la Kujenga Uwezo, Bi. Martha Makoi (wa pili kushoto), Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Ushirikishwaji wa Wazawa na Uhusishwaji wa Wadau kutoka PURA, Bw. Ebeneza Mollel (wa pili kulia) na Bw. Hakeem Mwaruka kutoka PURA katika picha ya pamoja mara baada ya kikao.

****************

Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) imekutana na kufanya mazungumzo na Kampuni ya Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) - upande wa Tanzania kwa lengo la kubadilishana uzoefu katika eneo la kuongeza ushiriki wa wazawa kupitia programu za kujenga uwezo. Mazungumzo hayo yalifanyika tarehe 11 Aprili 2023 katika Ofisi za EACOP Jijini Dar es Salaam. Miongoni kwa waliohudhuria kikao hicho ni Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Ushirikishwaji wa Wazawa na Uhusishwaji wa Wadau kutoka PURA, Bw. Ebeneza Mollel na Meneja wa Ushiriki wa Wazawa kutoka Kampuni ya EACOP, Bw. Olivier Foulonneau.

Akiongea katika kikao hicho, Bw. Ebeneza alieleza kuwa, miongoni mwa mikakati inayotumiwa na PURA kuongeza ushiriki wa watanzania katika shughuli za mkondo wa juu wa petroli ni kuwafikia na kuwashirikiana na wadau mbalimbali wa sekta hiyo. Kupitia mashirikiano hayo, PURA hupata mawazo ya wadau juu ya jinsi ya kuongeza ushiriki wa watanzania na kupata kusikia changamoto zinazowakabili wadau hao wakati wa utekelezaji wa matakwa ya kisheria ya ushiriki wa watanzania.

“PURA inaamini kuwa, suala la kuongeza ushiriki wa watanzania linahitaji juhudi shirikishi ili kufikia matokeo yanayotarajiwa. Kwa kuwa EACOP ni mmoja wa wadau wenye mchango mkubwa katika kuongeza ushiriki wa watanzania, PURA iliona ipo haja ya kukutana na kampuni hii kubadilishana uzoefu katika suala hili” aliongeza Bw. Ebeneza.

Kwa upande wake, Bw. Oliver alisema ni heshima kubwa kuwa na mazungumzo na PURA kama mmoja wa wadau kujadili suala la ushiriki wa watanzania ikiwemo jitihada zinazofanywa na Kampuni ya EACOP katika eneo hilo.

“Kampuni ya EACOP, mbali na kuhakikisha kuwa wakandarasi wakuu wa mradi wanazingatia matakwa ya ushiriki wa watanzania kama yalivyoainishwa katika Mkataba wa Nchi Hodhi na Kanuni za Ushiriki wa Watanzania za mwaka 2017; Kampuni imekuwa ikifanya programu mbalimbali za kuwajengea uwezo watanzania na watoa huduma wakitanzania” aliendelea bwana Olivier.

Akifafanua zaidi kuhusu mikakati inayotekelezwa EACOP Tanzania katika kuwajengea uwezo watanzania, Afisa anayehusika na masuala ya kujenga uwezo, Bi.Martha Makoi alisema kuwa kampuni hiyo inashirikiana na vyuo mbalimbali vya ufundi stadi kama vile Chuo cha Ufundi Arusha na Taasisi ya Teknolojia Kilimanjaro (KIITEC). Mashirikiano haya yatawezesha vyuo hivyo kuwa na uwezo wa kuzalisha wataalamu watakaohitajika katika Mradi wa EACOP (upande wa Tanzania).

Mradi wa EACOP unahusu ujenzi wa bomba la mafuta lenye urefu wa kilomita 1,443 litakalosafirisha mafuta ghafi kutoka maeneo ya Ziwa Albert nchini Uganda hadi Bandari ya Tanga nchini Tanzania ambapo mafuta hayo yatauzwa katika masoko ya nje. Kwa upande wa Uganda, bomba litapitia wilaya 10 na kaunti 25 na litakuwa na jumla ya kilomita 296. Nchini Tanzania, bomba litakuwa na urefu wa kilomita 1,147 na litapita katika mikoa 8 na wilaya 25. Utekelezaji wa mradi huu utaleta na fursa nyingi zikiwemo ajira na ugavi wa bidhaa na huduma.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments