MTATURU AIKUMBUSHA SERIKALI UJENZI WA BARABARA




MBUNGE wa Singida Mashariki Miraji Mtaturu,ameiomba serikali kuweka mkazo katika ujenzi wa barabara zinazounganisha mikoa ambazo utekelezaji wake ulipitishwa katika bajeti ya 2022/2023.

Barabara hizo ni ya kutoka Tanga kwenda Singida hadi Mkiwa kwa maana ya Itigi mpaka Mbeya.

Akichangia April 13,2023 mjadala wa bajeti ya ofisi ya waziri mkuu kwa mwaka 2023/2024,bungeni Jijini Dodoma Mtaturu amesema barabara hiyo iliwekwa kwenye bajeti inayoishia lakini utekelezaji wake bado haujaanza.

“Sisi watu wa Singida bado tuna changamoto ya kuunganisha barabara na mikoa, na kuna maeneo mawili bado hatujaunganishwa ambayo ni barabara ya kutoka Tanga kuja Singida hadi Mkiwa kwa maana ya Itigi mpaka kwenda Mbeya,lakini tunafuraha kuwa tuliwekwa kwenye bajeti inayoishia na tuliahidiwa kujengewa Kilomita 2,100,

Ameeleza kuwa barabara ya Itigi hadi Makongorosi mpaka kule Mbeya,barabara hiyo bado haijapata mkandarasi na barabara ya Singida kwa Mtoro kwenda Kiblashi Tanga nayo haijaanza ujenzi.

“Zikikamilika barabara hizi zitaongeza uchumi wa wananchi wetu,zitaongeza thamani ya miradi tunayoitengeneza, mfano barabara ya Tanga itahuisha bandari ya Tanga ambayo imewekezwa fedha nyingi sana,tuliambiwa tutatumia mfumo wa EPC plus F lakini mpaka leo tunavyoongea bado wapo kwenye mazungumzo hawajamaliza hatua za manunuzi,”ameongeza.

Amesisitiza kuwa wananchi wanasubiri barabara hizo kwa hamu kwa sababu serikali ilishaahidi kwenye mwaka wa fedha unaoisha.

Akizungumzia suala la ajira Mtaturu ameishukuru serikali kwa kazi nzuri wanayoendelea kuifanya ya kuajiri na kuomba wahitimu wa mwaka 2015,2016 hadi 2020 kupewa kipaumbele katika ajira mpya 21,200 zilizotangazwa jana.

“Tumekuwa na hao wahitimu wamekuwa wakiomba nafasi ajira zikitoka lakini hawapati,wameshakaa mtaani vya kutosha,tunaomba sasa kwenye ajira hizi wapewe kipaumbele cha kuajiriwa ili wasiondoke kwenye muda wa utumishi maana wakichelewesha kwenye miaka mitano ijayo watakuwa hawaajiriki na itakuwa haina sababu ya kuwasomesha kwa fedha nyingi na wengine wamekopa bodi ya mikopo ya elimu ya juu,”ameomba.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments