MCHENGERWA AWAONGOZA WANARUFIJI KUFANYA DUA MAALUM LA KUMWOMBEA MHE. RAIS SAMIA NA TAIFA, AWAFUTURISHA ZAIDI YA WANANCHI 8000.Na John Mapepele

Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM kupitia Mkoa wa Pwani ambaye ni Waziri wa Maliasili na Utalii na Mbunge wa Rufiji, Mhe. Mohamed Mchengerwa amewafuturisha zaidi ya waumini 8000 wa dini ya kiislam wa Wilaya ya Rufiji, huku akiungana na waumini hao kufanya dua maalum ya kumwombea Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan na Taifa kwa ujumla katika kipindi hiki cha mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Mhe. Mchengerwa ametoa sadaka ya futari na dua hiyo kwa siku mbili mfululizo Aprili 8 na 9 mwaka huu, kwenye eneo la Utete na Ikwiriri ambapo dua hizo ziliongozwa na Shekh maarufu nchini, Shekh Kipozeo.

Mbali na Shekh Kipozeo pia mashehe wengine na viongozi mbalimbali Waandamizi wa Serikali na Wabunge ikiwa ni pamoja na Mke wa Rais Mstaafu, Mama Salma Kikwete wameshiriki katika tukio la kihistoria katika wilaya ya Rufiji ambapo kwa upande wake Mama Kikwete amepongeza kazi kubwa inayofanywa na Mhe. Mchengerwa na Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuwaletea maendeleo wananchi wa Mkoa wa Pwani na Tanzania kwa ujumla wake.

Mhe.Mchengerwa amefafanua kwamba ibada ya funga katika mwezi huu Mtukufu wa Ramadhani ni muhimu kuendana na ibada ya kufanya kazi kwa bidii.

“Ibada ya funga inaendana na Ibada nyingine, mfungo wa ramadhani ni miongoni mwa nguzo tano za kiislam ambazo Mwenyezi Mungu amezishusha kwa waumini, lakini kushuka kwa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani hakutukatazi waislam kufanya kazi hivyo nawaombeni ndugu zangu tufanye kazi kwa bidii ili kupata chakula, ajira na kuinua uchumi wa nchi yetu” amesisitiza Mhe. Mchengerwa.

Aidha, Mhe. Mchengerwa amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha nyingi ambazo zimesaidia kuboresha huduma zote za jamii katika Wilaya hiyo.

Amazitaja huduma hizo zilizoboreka kuwa ni pamoja na ujenzi wa shule nyingi za Sekondari, Zahanati, miundombinu ya Barabara na Madaraja ambayo yameunganisha mikoa ya kusini na mikoa mingine pia kuunganishwa kwa umeme ambapo amefafanua kuwa Rufiji inakwenda kuwa miongoni mwa Wilaya ambazo nimeunganishwa na umeme kwa asilimia kubwa.

Ametoa wito kwa wananchi wa Wilaya ya Rufiji kuendelea kumwombea Rais Samia Suluhu na Serikali yake ili iendelee kuwaletea maendeleo.

Mhe. Mchengerwa amekuwa akitoa sadaka ya kufuturisha waumini na wasio waumini wa dini ya kiislam kwa zaidi ya miaka mitano mfululizo katika kipindi cha mwezi Mtukufu wa Ramadhan huku akifafanua kuwa ni sadaka yake kurejesha riziki kwa wanarufiji kwa namna ambazo Mwenyezi Mungu alivyomjalia.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post