MCHENGERWA ATOA WITO KWA WATANZANIA KUTEMBELEA VIVUTIO VYA UTALII WAKATI WA PASAKA NA IDD


Na John Mapepele

Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mohamed Mchengerwa ametoa wito kwa watanzania wote kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii wakati wa sherehe za Pasaka na Iddi huku akiwatakia heri katika sherehe hizo.

Mhe. Mchengerwa atoa wito huo leo ambapo amesema Tanzania imebarikiwa kuwa na vivutio vizuri kwa ajili ya watu kutembelea na kuona urithi na utajiri wa vivutio mbalimbali.

Amesema kwa kufanya hivyo watanzania watakuwa wanaanzisha utamaduni mzuri wa kuthamini raslimali za kwao lakini kubwa zaidi watakuwa wanachangia kwenye uchumi wa nchi kama watalii wa ndani.

Aidha amesema gharama za kuyatembelea maeneo haya zipo chini zikilinganishwa na maeneo mengine duniani.

Waziri Mchengerwa ameyataja baadhi ya maeneo ya Utalii hapa nchini mbuga na Hifadhi za taifa, makumbusho ya taifa, maeneo yaliyohifadhiwa ya misitu ambayo yanatamba kwa Utalii wa ikolojia.

Aidha, amesema kwa upande wa utalii wa baharini, tayari Wizara kupitia Mamlaka ya Wanyamapori nchini (TAWA) wameleta Bodi ya kitalii yenye kioo chenye lensi maalum inayomfanya mgeni kuona viumbe mbalimbali wa majini hata kama hawawezi kuogelea.

Kwa upande wa uhifadhi wa raslimali, Mhe. Mchengerwa amewataka watendaji wa taasisi zote zilizochini ya Wizara kushirikiana na wananchi wanaozunguka maeneo yaliyohifadhiwa katika kuhifadhi ili kazi hiyo iwe na tija.

Amesema raslimali zilizohifadhiwa zinatakiwa kuhifadhiwa kwa faida ya kizazi cha sasa na baadaye hivyo elimu zaidi inatakiwa kutolewa ili jamii inayozunguka iwe sehemu ya uhifadhi huo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post