LHRC YAZINDUA RIPOTI YA HAKI ZA BINADAMU YA MWAKA 2022, YAIPONGEZA SERIKALI


*********************

NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) wameipongeza Serikali kwa kuimarisha uhuru wa vyombo vya habari ikiwemo kwa kuvifungulia vyombo vinne vya habari vilivyokuwa vimefungiwa.

Pongezi hizo zimetolewa leo Aprili 12,2023 na Mkurugenzi Mtendaji LHRC, Wakili Anna Henga kwenye uzinduzi wa Ripoti ya Haki za Binadamu ya mwaka 2022 ambayo imefanyika kwa njia ya mtandao kwa kuwajumuisha waandishi wa habari mbalimbali.
Amesema licha ya Serikali kufanya vizuri kwenye suala hilo lakini bado kuna sheria mbalimbali ambazo zina vifungu vinavyominya uhuru wa vyombo vya habari, ikiwemo Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016.

"Tunafurahi pia kuondolewa kwa katazo la mikutano ya kisaisa ya hadhara hivi karibuni, ambalo lilikuwa linakiuka uhuru wa kujumuika na kukuanyika kwa muda mrefu, ikiwemo mwaka 2022.

Aidha amesema katika upande wa vitendo vya ukatili, tathmini walioifanya inaonyesha watoto walikuwa ni wahanga wakuu wa vitendo hivyo (47%), wakifuatiwa na wanawake (33%), na wazee (10%), watu wenye ulemavu (4%), na wengine, ikiwemo wanaume, (6%), hivyo kukiuka haki ya uhuru dhidi ya ukatili.

Amesema Matukio ya wananchi kujichukulia sheria mkononi yameendelea kuwa mwiba kwa haki ya kuishi, ambapo kwa mwaka huu LHRC imekusanya matukio 40, ambayo ni 18 zaidi ukilinganisha na mwaka 2021.

Hata hivyo amesema kuwa matukio ya mauaji yanayotokana na imani za kishirikina yamepungua, lakini bado ni changamoto, hasa kwa wanawake, ambao walikuwa ni 52% ya wahanga.

"Mashambulio na mauaji ya watu wenye ualbino pia yameibuka upya miaka ya hivi karibuni, na mwaka 2022 lilitokea tukio jingine la mauaji ya mtu mwenye ualbino mkoani Mwanza, ambaye alifariki baada ya kukatwa mkono. Mauaji ya mwenza yanayofanywa na mwenza pia yameendelea kuathiri haki ya kuishi yakisababishwa na wivu wa kimapenzi". Amesema

Amesema Haki ya usawa mbele ya sheria imeandelea kuwa mojawapo ya haki zinazokiukwa zaidi kwa sababu ya vikwazo mbalimbali vya upatikanaji haki na changamoto katika mfumo wa haki jinai.

"Mojawapo ya vikwazo vikubwa vya upatikanaji haki kwa mtazamo wa wanajamii ni rushwa (82%), ikifuatiwa na kesi kuchukua muda mrefu na uelewa mdogo kuhusu sheria (54%)". Amesema

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments