DITOPILE AGAWA FUTARI KONDOA, ASISITIZA KUIOMBEA NCHI NA KUMUOMBEA RAIS SAMIA


Katika Muendelezo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani, Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Dodoma Mhe. Mariam Ditopile amegawa Futari kwa Wazee, Wajane na watu wasio jiweza Wilaya Kondoa Mkoani Dodoma.


"Kwa imani yetu miezi yote ni bora lakini mwezi mtukufu wa Ramadhani ni bora zaidi, na pia tunaambiwa katika mwezi huu dua yoyote utakayoiomba mbingu ziko wazi na Mwenyezi Mungu ametukumbusha kupitia suratul Insan aya ya 8 tuwafuturishe kile tunachokipenda",amesema
Ameongeza kuwa huu ni utaratibu ambao anautumia mwezi huu mzima kuzunguka Mkoa wa Dodoma kufanya zoezi hilo.


"Nimetumia mwezi huu wa Ramadhani kuzunguka Mkoa wote wa Dodoma kufuturisha, nimeanza pale Dodoma mjini kwa kufuturu na yatima na wajane zaidi ya 300 na kisha kuwapa sadaka, nimeshafuturisha wilaya za Bahi, Kongwa na leo nipo Kondoa. Pale Kongwa nilienda kijiji cha Mkoka pamoja na futari na nilienda kutembelea shule ya watoto wenye uhitaji maalum, ambako wapo watoto wadogo wenye ulemavu lakini walikuwa wamefunga",amesema.


Pia Mbunge Ditopile amewaomba kuendelea kuiombea Nchi na kumuombea Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan."Sisi ni viongozi mmetuamini lakini juu yetu yupo Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, mama Samia amepewa majukumu ya kutuongoza na Mwenyezi Mungu, hata majukumu yake ya kifamilia ameyasahau kidogo na muda mwingi anahangaika na wananchi wa Kondoa, Kasulu na kila mahali nchini leo, anawaza leo nipeleke mradi wa maji wapi, leo nipeleke mradi wa umeme wapi ni na dhamira yake njema ya kuwatumikia Watanzania wapo ambao hawaipendi, hasad haikosekani katika jambo lolote linaloambatana na neema, ili hasad isimkute ni jukumu letu sote kumuombea kwa Mwenyezi Mungu",amesema


Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Dodoma Mhe Mariam Ditopile anaendelea kuwatakia Waislamu wote nchini Ramadhani njema.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post