AUAWA KWA KUPIGWA JIWE AKINYWA POMBE BAA MJINI SHINYANGA, MWINGINE AKIIBA MAHINDI SHAMBANI


Kaimu Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga kamishna msaidizi wa Polisi Leonard Nyandahu

Na Mapuli Misalaba, Shinyanga

Watu wawili wamefariki Dunia katika matukio mawili tofauti yaliyotokea katika Manispaa ya Shinyanga likiwemo la mwanaume kuuawa akiiba mahindi shambani na mwingine kupigwa jiwe akiwa Baa.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kaimu Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga kamishna msaidizi wa Polisi Leonard Nyandahu amewataja watu hao kuwa ni Tumaini Manyele Malima mwenye umri wa miaka 35 mkazi wa mtaa wa Kambarage Manispaa ya Shinyanga na mwanaume mwingine anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 35 mpaka 40 ambaye hakufahamika jina na makazi yake.
Amesema Tumaini Malima amefariki dunia akiwa anapatiwa matibabu Hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Shinyanga Mwawaza baada ya kujeruhiwa kwa kupigwa jiwe katika sikio la kushoto na Yohana Daniel akiwa Bar ya Heinken mjini Shinyanga wakiendelea kunywa pombe kisha kuanza kupigana.

Kaimu Kamanda Nyandahu amesema tukio la pili ni kuhusu mwanaume anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 35 – 40 ambaye hakufahamika jina wala makazi yake ameuawa kwa kushambuliwa baada kukamatwa na wananchi kwa tuhuma za kuiba Mahindi mabichi shambani katika kijiji cha Mwamalili kilichopo Manispaa ya Shinyanga usiku wa kuamkia leo Aprili 4,2023.

Kaimu Kamanda wa Jeshi la polisi Mkoa wa Shinyanga Leonard Nyandahu ametoa wito kwa wananchi kuacha tabia ya kujichukulia sheria mkononi na badala yake kutoa taarifa kwa jeshi la polisi pindi matukio ya uhalifu yanapotokea.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post