SHIRIKINI KWENYE MIRADI ILI MUWEZE KUIMILIKI NA KUIVUTIA SERIKALI KUIENDELEZA - MBUNGE  MTATURU

Na Mathias Canal, Ikungi- Singida

Mbunge wa Jimbo la Singida Mashariki Mhe. Miraji Jumanne Mtaturu amewataka wananchi wa Wilaya ya Ikungi kushiriki kwenye shughuli za maendeleo ikiwa ni pamoja na kutunza miradi inayotekelezwa na serikali katika maeneo yao.

Mhe. Mtaturu amesema hayo jana April 15 katika shule ya Sekondari Ikungi wakati akizungumza na Waumini wa Kiislamu na pamoja na wananchi wa Ikungi kwenye hafla ya Futari alioandaa kwa watu wenye uhitaji katika mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Amesema kuwa ili wananchi waweze kuwa na uchungu na miradi inayotekelezwa na serikali wanapaswa kushiriki katika miradi hiyo huku akimpongeza Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kufungua diplomasia ya Uchumi ambapo Wilaya ya Ikungi imenufaika na fursa hiyo.

“Wakati nakuja hapa 2016 wananchi walikuwa hawashiriki kwenye shughuli za maendeleo lakini juzi tumeleta mradi wananchi wamemiminika wanakwenda kushiriki kwenye Maendeleo, Shirikini miradi yenu Muimiliki serikali kweli italeta lakini na wewe shiriki ukiwa una jambo unaomba serikali ifanye anza wewe ule mradi uone kuwa na wewe unauhitaji”. Alisema Mhe Mtaturu.

“Katika kipindi ambacho kila kijiji kina mradi ni sasa , leo kila kijiji ukienda ikungi utakuta mradi kama sio shule ni zahanati , kama sio zahanati ni barabara kama sio barabara ni umeme kama sio umeme ni maji maana yake huku chini kwa wananchi shughuli zinaendelea” Alisema Mhe. Mtaturu.

Aidha Mbunge huyo amewausia waumini hao pamoja na wananchi walioshiriki futari hiyo kuwe wanyenyekevu na kumjua Mwenyezi Mungu kwa kutangulia mazuri ambayo yatakuwa mtaji mbele za Haki.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Baraza la Waislamu Tanzania Mkoa wa Singida Alhaj Burhan Mohamed Mlau amempongeza Mbunge huyo kwa kuwajali wenye uhitaji kwenye futari hiyo na kuongeza kuwa kwa kuwahimiza waumini wa dini ya Kiislamu kuendeleza mema ambayo wanafanya kwenye mwezi huu mtukufu wa Ramadhani.

Alhaj Mlau ametumia nafasi hiyo kutoa Wito kwa wadau wengine wenye uwezo kuwafuturisha na kuwajali wenye utahitaji ikiwa ni pamoja na Yatima, Maskini, wajane, wafungwa waliopo magerezani.

“Tuwaombe wenye uwezo wawafuturishe au wawasaidie wale ambao hawana uwezo kwa maana ya walengwa kama vile Yatima, Maskini, Wajane, Mafukara na Wazee wawasaidie kama una uwezo ili kushirikiana kama hawa watoto walemavu Mheshimiwa amekusanya … Kwahiyo kwa niaba ya Baraza la Waislamu Mkoa wa Singida na waiislamu kwa ujumla tunakushukuru sana Mheshimiwa uendelee na moyo huo” Alisema Alhaj Mlau.

Futari hiyo imehudhuriwa na Viongozi wa wa dini mbalimbali Mkoa wa Singida, Viongozi wa chama na Serikali, na Wazee maarufu ikiwa na lengo la kuwasaidia wenye uhitaji na kuwaleta pamoja ambapo zawadi mbalimbali zimetolewa kwa watoto wenye ulemavu na wanafunzi wa shule ya Msingi na Sekondari Ikungi.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments