OSHA YAIMWAGIA SIFA BENKI YA CRDB KWA KUZINGATIA USALAMA MAHALI PA KAZI


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Profesa Joyce Ndalichako akimkaidhi tuzo Mkuu wa kitengo cha Ulinzi, Usalama na Mwendelezo wa Biashara wa Benki ya CRDB, Misana Mutani wakati Benki ya CRDB ikitunukiwa tuzo tatu ambazo ni mshindi wa kwanza katika kundi la benki na taasisi za fedha katika utekelezaji wa sera za Osha, Tuzo nyingine ni ya ufanisi katika utoaji huduma bora unaozingatia afya na usalama wa kazi kwa benki na ile ya kamati bora ya Osha katika huduma za kibenki, wakati wa kilele cha maadhimisho ya Siku ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi Duniani ambayo kitaifa yalifanyika mkoani Morogoro.
Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi nchini (OSHA) umeipongeza Benki ya CRDB kwa kuwa mfano kwa taasisi za fedha katika kuzingatia na kujali usalama na afya kwa wafanyakazi wake.


Pongezi hizo zimetolewa na Mtendaji Mkuu wa OSHA Bi Khadija Mwenda kwenye kilele cha maadhimisho ya Siku ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi Duniani ambayo kitaifa yalifanyika mkoani Morogoro. Kwenye kilele cha maadhimisho hayo Benki ya CRDB ilipewa tuzo kwa kuzingatia viwango vinavyokubalika kwa usalama na afya za wafanyakazi wake.

“Naipongeza taasisi hii kubwa ya fedha nchini kwa kuwa mfano katika kuzingatia suala zima la usalama mahali pa kazi. Napenda kuchukua nafasi hii kuzitaka taasisi nyingine nazo kuiga mfano huu ili kuimarisha usalama na afya mahali pa kazi kwa wafanyakazi wao,” alisema Bi Khadija.

Aidha, alisema lengo la maadhimisho hayo ni kuuhamasisha umma kuhusu usalama na afya mambo wanayoyasimamia chini ya sheria namba tano ya mwaka 2003 na kuhakikisha hilo linazingatiwa OSHA imekuwa ikifanya maadhimisho yanayohusisha kuwakumbuka wafanyakzi waliopoteza maisha au kuathirika wakiwa kazini na kuonyesha namna ya kuboresha usalama sehemu za kazi na jinsi zinavyoweza kusimamiwa katika kuhakikisha usalama kwa wafanyakazi wote.


Kwa upande wake Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Profesa Joyce Ndalichako aliyekuwa mgeni rasmi kwenye maadhimisho hayo alisema serikali inatambua na kuthamini usalama na afya mahali pa kazi.

“Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inatambua usalama na afya mahali pa kazi ni haki ya msingi ya kila mfanyakazi nchini na ndiyo sababu Rais amekuwa mstari wa mbele kuhakikisha nguvukazi ya taifa inalindwa,” alisema Profesa Ndalichako.

Waziri Ndalichako alisema kutokana na hilo serikali kupitia OSHA inaendelea kusimamia kwa karibu sheria namba tano ya afya na usalama mahali pa kazi ya mwaka 2003 kuhakikisha maeneo yote ya kazi yanakuwa na mifumo madhubuti ya kuwalinda wafanyakazi kutopata ajali au kuambukizwa magonjwa.

Aidha aliwapongeza wadau walioshiriki maadhimisho hayo ikiwemo Benki ya CRDB na kuwataka kuongeza usimamizi wa usalama na afya mahali pa kazi kwenye taasisi zao.

Mkuu wa kitengo cha Ulinzi, Usalama na Mwendelezo wa Biashara wa Benki ya CRDB, Misana Mutani alisema ufanisi mzuri wa benki hiyo ndiyo uliozaa matunda ya wao kupewa tuzo tatu katika kuzingatia afya na usalama mahali pa kazi kwa wafanyakazi.
Mutani alisema CRDB sio tu inazingatia usalama wa wafanyakazi wake pekee bali jamii inayowazunguka kwa maana ya wateja na wageni wanaotembelea maeneo ya benki hiyo kwani inahakikisha wapo salama wakati wote. Mbali na kuzingatia afya na usalama mahali pa kazi, alisema benki pia huendesha mbio za hisani maarufu kama CRDB Marathon ambazo hufanyika kila mwaka kwa mafanikio makubwa ili kukusanya fedha ambazo husaidia matibabu ya watoto wenye matatizo ya moyo au wanawake wenye fistula.

Mutani alisema fedha zilizokusanywa zimewezesha upasuaji wa watoto waliotibiwa katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), kuwatibu wanawake waliokuwa na fistula waliotibiwa katika Hospitali ya CCBRT na kujenga kituo cha huduma kwa njia za simu “Call Center” katika Hospitali ya Ocean Road Ili kurahisisha upatikanaji wa taarifa sahihi kwa mgojwa kupata huduma bila kulazimika kusafiri kuja kupata taarifa.

“Kwa ujenzi wa kituo kile sasa wagonjwa wanaweza kuweka miadi au kupata taarifa za awali bila kulazimika kusafiri umbali mrefu hivyo kuwapunguzia gharama ambazo hapo awali walikuwa wanashindwa kuzimudu," alisema Mutani.


Naye Meneja na Usaidizi wa Huduma wa CRDB, Elia Mnonjela alisema wakati anaongea na wadau waliotembelea banda lao katika maonyesho hayo wamefahamishwa kuhusu huduma nafuu zinazowapa fursa ya kujikwamua kiuchumi.

"Tunayahudumia makundi yote yaani wafanyakazi na wafanyabiashara. Kwa unafuu uliopo, wafanyakazi wana wigo mpana zaidi wa kukopa katika benki yetu na kukuza uchumi wao kwa riba nafuu tofauti na awali," alisema Mnonjela.

Kwenye maadhimisho hayo Benki ya CRDB ilitunukiwa tuzo tatu. Ya kwanza ni mshindi wa kwanza katika kundi la benki na taasisi za fedha katika utekelezaji wa sera za Osha. Tuzo nyingine ni ya ufanisi katika utoaji huduma bora unaozingatia afya na usalama wa kazi kwa benki na ile ya kamati bora ya Osha katika huduma za kibenki.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post