Waziri wa nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu George Simbachawene akizindua Mpango shirikishi wa Taifa wa kuzuia kipindupindu jijini Dodoma.
Na Dotto Kwilasa, Malunde1 Blog DODOMA
SERIKALI kupitia Ofisi ya Wa Mkuu,Sera, Bunge na Uratibu imezindua mpango shirikishi wa Taifa wa kuzuia na kukabiliana na kipindupindu 2023/2027 huku ikitangaza uwepo wa mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu ambapo kuanzia Februari 19 hadi Machi 15 mwaka 2023 imepokea taarifa ya wagonjwa 60 Kutoka mikoa 4 ya Tanzania Bara.
Akiongea kwenye uzinduzi wa Mpango Shirikishi wa Taifa wa Kuzuia na Kukabiliana na Kipindupindu , Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera,Bunge na Uratibu George Simbachawene ametumia nafasi hiyo kuitaka Wizara ya afya kuongeza nguvu ya ufuatiliaji ili kuhakikisha wagonjwa na tetesi zote zinatolewa taarifa kushughulikiwa mapema kwenye vituo vya afya kabla ugonjwa haujasambaa .
Waziri Simbachawene ameitaja mikoa hiyo yenye wagonjwa wa kipindupindu kuwa ni pamoja na Ruvuma mgonjwa 1, Kigoma 7, Katavi 34 na Rukwa18.
"Hivi karibuni baadhi ya mikoa kama Katavi, Kigoma, Ruvuma, Manyara na Rukwa imekuwa ikipata milipuko ya Kipindupindu katika baadhi ya Halmashauri zake,ni hatari na aibu,ugonjwa huu unachukuliwa kama umaskini kutokana na namna unavyoanza,"amesema
Amesema kuwa ugonjwa wa kipindupindu kama yalivyo magonjwa mengine ya mlipuko, unasambaa kwa kasi na wakati mwingine kuvuka hata mipaka ya nchi.
" Taarifa kutoka shirika la Afya Dunia inaeleza kuwa na mlipuko mkubwa wa Kipindupindu nchini Malawi ambapo hadi kufikia tarehe 15 Machi 2023 kulikuwa na jumla ya wagonjwa 53,925 na vifo 1,658 vilivyotolewa taarifa"amesema na kuongeza;
Hii inatupa tahadhari ya mlipuko huo pia kuvuka mipaka na kuingia nchini kwetu hususani pale tusipo imarisha afua mbalimbali za kujikinga na kipindupindu kwa jamii zetu hususani kwa Mikoa inayopakana na nchi hiyo" amesisitiza
Pamoja na hayo amesema tetesi za kuwepo kwa mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu pia zipo kwa nchi nyingine zinazo pakana na Tanzania ikiwemo Msumbiji, DRC Congo, Zambia na Kenya .
"Ni mategemeo yangu kuwa Mikoa hii na Nchi nzima kwa ujumla imejiandaa vyema kuhakikisha kuwa ugonjwa huo kwanza unazuiwa lakini pia unakabiliwa pale utakapokuwa umevuka mipaka na kuingia kwetu,"amesema
Simbachawene pia ametoa wito kwa ngazi zote za utekelezaji kuhakikisha kuwa shughuli zote zilizopangwa kwenye mpango huo zinatekelezwa kwa wakati na weledi mkubwa ili matokeo yake yaweze kuwa chanya katika kuzuia na kukabiliana na ugonjwa huo hatari, hususan kwenye maeneo yenye kupata milipuko ya Kipindupindu mara kwa mara.
"Natumia nafasi hii kuwaomba wadau wote wa maendeleo kuendelea kufanya kazi na serikali katika kutekeleza mpango huu ili kuhakikisha ugonjwa huo unazuia kabisa au kuhakikisha madhara yake yanapunguzwa kabisa,ushirikiano wenu unahitajika katika kutekeleza shughuli zote zinazohusiana na kipindupindu,"amesisitiza .
Wakati huo huo amezitaka Ofisi za tawala za Mikoa na Halmashauli zote kushirikiana na mamlaka za maji mijini na vijijini (RUWASA) kuhakikisha hali ya upatikanaji wa maji katika maeneo yao inaimarika.
Vilevile amezitaka mamlaka za maji kupitia jumuiya za watumia maji kutibu maji kabla ya kuyasambaza, kuchukua sampuli za maji kila mara kutoka katika vyanzo tofauti na kuyapima katika maabara za mikoa za ubora wa maji, kuhimiza wananchi kujenga vyoo bora na kuvitumia na kuviweka katika hali ya usafi.
"Ofisi za Serikali za Mikoa na Halmashauri zote ziendelee kutoa elimu kwa wananchi kuepuka uchafuzi wa vyanzo vya maji kwa kuoga, kufua, kutupa takataka ovyo na kadhalika ,Ushirikiano wa kisekta unahitajika katika kutekeleza shughuli zote zinazohusiana na kipindupindu,"amesema
Naye mwakilishi mkazi wa Shirika lisilo la kiserikali la SAVE THE CHILDREN Angela Kauleni amesema juhudi za pamoja bado zinahitajika Katika mapambano ya magonjwa ya mlipuko na kwamba shirika hilo litaendelea kupambana na magonjwa hayo kuhakikisha watoto wanakuwa salama na jamii kwa ujumla.
Amesema katika kukabiliana na kipindupindu shirika hilo linafanya juhudi kutoa mafunzo ya mara kwa mara kwa watoa huduma ngazi ya Jamii na ufuatiliaji wa kanuni za afya kwa Jamii ikiwa ni pamoja na kuelimisha jamii kanuni Bora za afya.
"Tumekuwa tukishirikiana na Ofisi za baadhi ya waganga wakuu kuelimisha wananchi kuepuka kutupa takataka ovyo na kuwahimiza kula vyakula vya moto na Usafi wa mazingira Kwa ujumla lengo letu kuhakikisha wananchi wanaacha tabia ya kutiririsha maji ya vyoo kwenye mifereji ya wazi na tabia nyingine hatarishi,"amesema
Kwa upande wake Katibu Mkuu ,Ofisi ya Waziri Mkuu ,Sera, Bunge na Uratibu Jim Yonaz amrsema mpango huo umeandaliwa kwa kuzingatia mahitaji ya Sasa na baadae ili kutokomeza kabisa kipindupindu .
"Suala la kuzuia na kukabiliana na ugonjwa wa kipindupindu ni mtambuka hivyo Wizara za Serikali, Taasisi mbalimbali za Serikali na Binafsi, Mashirika yasiyo ya Kiserikali na yale ya Umoja wa Mataifa yanapaswa kishirikiana Kwa ukaribu,na sisi kama Serikali tutaendelea kutoa elimu Kwa jamii namna ya kuuepuka ugonjwa huu,"amesema