WAZIRI KIJAJI AITAKA TBPL KIBAHA KUWEKA MIKAKATI YA KITANGAZA DAWA YA KUUA VILUWILUWI VYA MBU

Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji pamoja na wajumbe wengine wakipewa maelezo na Jovin Magayane (mwenye koti jeupe), Mtaalam wa Maabara wa Tanzania Biotech Products Limited (TBPL) namna sampuli mbalimbali zinavyopimwa ndani ya maabara ya kiwanda hicho ili kuzalisha viuadudu vya kuangamiza mazalia ya mbu.'

*****************

Na.Mwandishi Wetu-PWANI

Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara Dk. Ashatu Kijaji (Mb.) amekitaka Kiwanda cha kutengeneza viuadudu (TBPL) kuhakikisha kinajitangaza ndani na nje ya nchi ili kuongeza wigo wa masoko kwa kuuza bidhaa hiyo ya kipekee ambayo inazalishwa hapa nchini.

Dk. Kijaji ameyasema hayo Machi, 29, 2023 alipotembelea kiwanda hicho kilichoko Kibaha Mkoani Pwani kushuhudia namna uzalishaji wa dawa za viuadudu unavyofanyika kiwandani hapo.

Akiwa kiwandani hapo Dkt. Kijaji amekiagiza kiwanda hicho kuhakikisha kinajitangaza kwa nguvu zote ili kupata masoko ya ndani na nje ya nchi badala ya kutegemea soko la ndani ambalo kwa kiwango kikubwa limeonekana kuwa ni la kusuasua.

“ Serikali imetimiza wajibu wake wa kuwekeza ili kuondokana na suala la Malaria hapa nchini na wajibu wetu ni kuhakikisha tunatoa elimu ya kutosha juu ya matumizi ya dawa hii kwa ajili ya kuua viluwiluwi vya Malaria ili kutimiza adhima ya Serikali ya kuondokana na malaria nchini". Alisitiza Dk Kijaji.

Aidha, Waziri Kijaji ameiagiza TBPL kushirikiana na TANTRADE katika kuhakikisha dawa hizo zinatangazwa katika masoko ya ndani na nje ya nchi pamoja na kuwa na mipango mikakati ya masoko itakayofanikisha utoaji wa elimu juu ya matumizi ya dawa hizo na faida zake kufika kwa watanzania wengi.

Awali akimkaribisha Mheshimiwa Waziri, Kaimu Mkurugenzi Mwendeshaji wa Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) ambayo ndio mmiliki wa kiwanda hicho Alfred Mapunda amesema NDC kwa kushirikiana TBPL wameanza utekelezaji wa mikakati mbalimbali ya kimasoko ikiwemo kuhakikisha mkataba wa mauzo baina ya NDC na Wizara ya Afya unasainiwa, pamoja na kuanza mchakato wa upatikanaji wa mawakala wa kuuza na kusambaza dawa hizo katika mikoa mbalimbali hapa nchini.

Katika hatua nyingine Mapunda pia alibainisha juu ya nia ya kiwanda hicho kuanza rasmi uzalishaji wa viuatilifu vya mazao ili kupambana na wadudu waharibifu wa mazao ambapo dawa hizo mara baada ya kufanyiwa majaribio zimeonyesha mafanikio makubwa katika kupambana na wadudu hao ambao ni hatari kwa ustawi wa sekta ya kilimo hapa nchini.

Akibainisha mafanikio ya kiwanda hicho Mapunda, amesema kimesaidia kwa kiwango kikubwa katika kushusha kiwango cha Malaria hapa nchini mathalani visiwani Zanzibar ambapo kutokana na matumizi ya dawa hizo kiwango cha maambukizi ya Malaria kimeshuka ambapo hivi sasa kipo chini ya asilimia moja, pamoja na upatikanaji wa masoko ya nchi za nje mathalani katika nchi za Msumbiji, Niger, Eswatin pamoja na Angola.

Kiwanda cha kitengeneza viuadudu cha TBPL kilichoko Kibaha mkoani Pwani ni kiwanda cha kipekee barani Afrika ambacho kinamilikiwa na serikali kwa asilimia mia moja kupitia Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) kikiwa ni mahususi katika kupambana na Maralia nchini na kina uwezo wa kuzalisha kiasi cha lita milioni sita kwa mwaka ambapo ujenzi wa kiwanda hiki ni matokeo ya ushirikiano wa kidiplomasia baina ya serikali ya Tanzania na Cuba.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post