UWT YATAKIWA KUBEBA AJENDA ZA WANAWAKE KITAIFA

 


Na Dotto Kwilasa,DODOMA

MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Abdulrahman Kinana ameitaka Jumuiya ya umoja wa Wanawake nchini(UWT)kubeba ajenda za kitaifa zinazowahusu wanawake wote kila wanapopata nafasi ya kuisemea Jumuiya hiyo.

Kinana aliyasema hayo  jijini hapa wakati akifungua mafunzo ya siku mbili ya  viongozi  wa Umoja wa Wanawake  Tanzania (UWT)ambayo yamehusisha viongozi 478 kuanzia ngazi ya Taifa hadi Wilaya.

Amesema  Kuna mambo ambayo hayaendi sawa sawa kwenye jamii na kuwaumiza wanawake na hivyo kuhimiza uongozi wa UWT kuwasemea Kila wanapopata nafasi .

"Nendeni mkabebe ajenda za kitaifa zinazowahusu wanawake wote nchini ,likitokea jambo ambalo wanawake hawaridhiki kuweni mstari wa mbele kuwasemea ,na sisi kama chama hatutawaacha nyuma,"amesema 

Akizungumzia uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 Kinana aliwataka wanawake kujitokeza kwa wingi kuwania nafasi mbalimbali za uongozi ili kufia lengo la kujenga jamii ya usawa.

Amesema mwakani kuna uchaguzi wa viongozi wa serikai za mitaa, ni vyema wanawake wakajitokeza kuchukua fomu kwa ajili ya kuomba nafasi mbalimbali za uongozi na CCM itawapa ushirikiano wa kutosha.

“Kuelekea uchaguzi ujao jiandaeni na kuwahimiza wanawake kuwania nafasi zote za uongozi na ninawahakikishia kuwa CCM itawaunga mkono kwa hali na mali ili kuwa na wanawake wengi waliochaguliwa katika majimbo,”ameisema

Kinana pia ametumia nafasi hiyo kuitaka UWT kuhakikisha maamuzi mengi yanafanyika kupitia vikao na sio maamuzi ya mtu mmoja au kikundi cha watu huku akisisitiza kwamba ndani ya chama hicho hakuna nani zaidi .

Amesisitiza kuwa hata kiongozi anapokosea sio busara kumuhamisha kituo cha kazi kabla ya kumuita na kumsikiliza kwani jambo hilo ni ukiukwaji wa haki na ni kinyume na maadili ya chama .

“Tumieni vikao kuamua mambo,niwakumbishe tu CCM haina nani zaidi Ila ina nani mwenzangu,  kila kitu lazima kijadiliwe kwa kina na kipite kwa hoja kwasababu ndani ya CCM hakuna maamuzi ya mtu mmoja au amri, na ninyi katika maeneo yenu hakikisheni ndani ya vikao huko ndio haki ya mtu itapatikana,”alisema

Kinana aliwataka viongozi hao kuto wahamisha hovyo viongozi kwani amebaini wengine wanashtukizwa bila kupewa taarifa ya uhamisho.

“Wenyeviti mpunguze kuhamisha watu hovyo kama mtu amekosea aitwe aelezwe kosa sio kuchukua maamuzi ya haraka una mualibia mtu mwelekeo, tujenge utamaduni wa kuambiana ukweli na msiogopane mtu anapokosea ,”alisema

Makamu huyo aliwashauri viongozi hao kusoma vitabu mbaimbali vya chama ikiweo Ilani ya uchaguzi,sera,kanuni  katiba vitawasaidia katika masuala mbalimbali ya uongozi.


Alisea CCM ni miongoni mwa vyama vichache duniani ambayo vinamaandishi mengi.

“Someni katiba, kanuni, ilani, na sera vitawasaidia kuendesha shughuli mbalimbali za chama na kuongoza kwa kuzingatia mingi ya haki,”alisema  

Kwa upande wake Mwenyekiti wa UWT Taifa Marry Chatanda alisema wanawake wanaridhika na kazi zinazofanywa na serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais Dk.Samia na ilani ya CCM inatekelezwa kwa kishindo.

Alisema katika kipindi cha miaka miwili ya serikali ya awamu ya sita hakuna kilichosimama ndio maana waliandaa hafla ya kumpongeza Rais Dk.Samia kwa kazi nzuri alizozifanya.

“Sisi wanawake wa CCM hakika tumeridhishwa na uongozi wa Rais Dk.Samia na tunaahidi katika uchaguzi wa mwaka 2025 tutatoa fedha kwa ajili ya kumchukulia fomu mwanamke mwenzetu,”amesema

Naye Katibu wa UWT Taifa Dk.Philis Nyimbi alisema lengo la mafunzo hayo ni kuleta ustawi na kuwapatia viongozi maarifa namna ya kuongoza jumuiya hiyo katika ngazi zote.

Alisema mafunzo hayo yamewakutanisha viongozi 478 ambapo baada ya kumaliza elimu waliyoipata wataipeleka katika ngazi ya kata na matawi.



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments