RAIS SAMIA AIFUNGUA TANZANIA KWENYE UTALII WA BAHARINI


👉Mhe. Mchengerwa kuzindua boti ya kisasa ya Utalii.

👉Meli tatu kumwaga watalii 400 wiki hii 

Na John Mapepele 

Kwa mara ya kwanza katika historia ya Tanzania, Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mohamed Mchengerwa Machi 14 mwaka huu anatarajiwa Kuzindua boti ya kisasa itakayotumika kwa ajili ya kufanya utalii wa baharini katika Bahari ya Hindi.

Upatikanaji wa boti hiyo ni jitihada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan katika kuhifadhi raslimali na kukuza utalii nchini ambapo Serikali yake imedhamiria kufikisha watalii milioni 5 na kuliingizia taifa pato la dola milioni 6 ifikapo mwaka 2025. 

Aidha, wakati Mhe. Mchengerwa anatarajia kuzindua meli hiyo ya utalii tayari meli tatu zinatarajia kutia nanga nchini zikiwa na takribani watalii 400 kutoka sehemu mbalimbali duniani wiki hii.

Meli hizo ni pamoja na Corals Geographic Cruise inayotarajia kuingia nchini kesho ikiwa na watalii 120, Le Jaques Cartier-Ponant yenye wageni 105 na Le Jaques Cartier- A & Luxury Expedition itakayoingia nchini Machi 14 mwaka huu ikiwa na watalii 138.

Aidha, Mhe. Mchengerwa amesema boti hiyo iliyotengenezwa nchini ni miongoni mwa boti za kisasa ambayo inamilikiwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) yenye vifaa vya kisasa vya kumfanya mtalii aweze kufurahia safari akiwa ndani ya boti hiyo.

Amesema boti hiyo imetengenezewa vioo vyenye lensi maalum ambazo vinamwezesha mtalii kuweza kuona viumbe mbalimbali wa baharini hata kama hawezi kuogelea. 

“Tunampongeza na kumshukuru Mhe.Rais wetu kwa kututafutia fedha ambazo zimeweza kununua boti hii ambayo ni ya kiwango cha kimataifa kabisa kwani sasa tuna matarajio makubwa kwamba Mhe. Rais anakwenda kuifungua Tanzania kwenye utalii wa baharini na tayari watalii wameshaanza kumiminika kuja kujionea vivutio vyetu vya utalii kwa upande wa baharini.”Amefafanua Mhe. Mchengerwa.

Mhe. Mchengerwa, amesema Serikali kwa kumiliki boti yake ya utalii itasaidia kuongeza na kukuza utalii wa ndani ambapo wananchi kutoka sehemu mbalimbali nchini wataweza kuja kutembelea na kujionea vivutio mbalimbali vya utalii ambavyo Tanzania imebarikiwa kuwa navyo ambavyo havipatikani sehemu nyingi duniani. 

Baadhi ya vivutio hivyo ni pamoja na viumbe ambao wapo kwenye orodha ya viumbe wa baharini ambao wapo hatarini kutoweka kabisa duniani (CITES) lakini Tanzania wanapatikana. 

Viumbe hao ni pamoja na Nguva, Potwe, Kasa na Silikanti ambao wote wameonekana katika eneo la bahari ya Tanzania. 

Tanzania inaaminika kuwa na mifumo ya bianuai mizuri ambayo ina bustani nzuri za matumbawe na aina nyingi za samaki kuliko sehemu nyingi duniani. 

Hadi sasa Tanzania Maeneo maalum yaliyohifadhiwa kama Hifadhi za Bahari matatu ambayo ni Hifadhi ya Bahari ya Kisiwa cha Mafia, Hifadhi ya Bahari ya Ghuba ya Mnazi na Maingilio ya Mto Ruvuma iliyopo mkoani Mtwara na Hifadhi ya Bahari ya Silikanti iliyopo Tanga. Pia kuna Maeneo Tengefu 15 yanayomilikiwa na Serikali ya Tanzania.

Amesema kuwa Boti hiyo inayofahamika la TAWA Sea Cruiser imetengenezwa na watanzania wazawa kupitia Kampuni ya Songoro Marine Transport Ltd inauwezo wa kuchukua takribani watalii 50 kwa wakati mmoja.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post