HISTORIA YA TEMBO DODOMA MBIONI KUTOWEKA

 

Kiongozi wa kimila wa Kabila la Wagogo chifu Mazengo wa II akiwaonyesha Waandishi wa habari za utalii Dodoma mti mkubwa aina Mkuyu ulivyotumika kunyongea wahalifu kipindi Cha ukoloni.
Baadhi ya Waandishi wa habari za utalii Dodoma wakiwa Katika picha ya pamoja na Chifu Mazengo wa II Katika eneo ambalo Tembo alizama  eneo ambalo Kwa Sasa limevamiwa na shughuli za kibinadamu.

Na Dotto Kwilasa, Malunde1 Blog-DODOMA.

WIZARA ya Mali asili na Utalii  imeshauriwa  kuweka alama kwenye maeneo yote ya hifadhi za kihistoria katika Mkoa wa Dodoma ili kuunga mkono juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan za kutangaza vivutio vya utalii na kuweka kumbukumbu kwa vizazi vijavyo. 

Hatua hiyo imekuja kufuatia baadhi ya wakazi wa Kikuyu Dodoma kutoa malalamiko kuwa vivutio vingi vya kihistoria mkoani hapo vimetelekezwa na havina usimamizi wa moja kwa moja kutoka Serikali zaidi ya ule wa kimila  na kusababisha shughuli za kibinadamu kuanza kufanyika kwenye maeneo hayo. 

Wakiongea  Jijini hapa, wakazi hao wamesema karibu maeneo mengi yanayobeba historia ya Mkoa wa Dodoma yametelekezwa na kuanza kupoteza uhalisia wake hivyo kushauri kuwepo namna ya kuweka kumbukumbu ya alama zitakazoonyesha umuhimu wake na kuwa kivutio.

Akitolea mfano wa kivutio ambacho ni muhimu na kinatakiwa kuwekwa alama Johnson Matiko amesema ni pamoja na eneo lililobeba asili ya neno Dodoma ambalo Tembo alididimia na kuzama moja kwa moja na kupelekea  wenyeji na wakazi wa eneo hilo lililopo Kata ya Kikuyu  kukiita kitendo hicho Idodomya yaani imedidimia na kupelekea Mkoa huo kuitwa Dodoma hadi leo.

"Mwanzoni eneo hili lĂ­liitwa Idodomya lakini kutokana na watalii wa kipindi cha ukoloni kushindwa kutamka neno hilo na kujikuta wakiita Dodoma na hapo ndipo neno hilo likaanza kuzoeleka na kutumika hadi sasa,hii ni historia na ni utalii ambao ulitumika vizuri utaiongezea mapato Serikali yetu na sisi wananchi wa kawaida,"amesema na kuongeza;

Tunashangaa kuona eneo hili limetelekezwa kiasi hiki mpaka watu wanaanza kujenga majengo yao,kifupi hakuna uhalisia hata mtu akitaka kuonyeshwa alipozama Tembo hawezi kuamini,tulitegemea ile juhudi ya Rais Katika utalii itaungwa mkono kwa kuweka uhifadhi wa maeneo ya Historia ya makao Makuu ya nchi lakini bado hakuna utekelezaji,"anasisitiza 
 
Ameongeza kuwa,watanzania tangu enzi za mababu wamekuwa wakifundwa na kusisitizwa kuipenda asili yao na kuijua kwa kina hivyo ni wajibu wao kuwa vinara wa kutunza asili ya utanzania na kuisemea pale wanapoona mambo yanaharibika ili vizazi vijavyo vifaidi na kuijua asili yao.

Kutokana na hayo Kiongozi wa kimila wa Kabila la Wagogo,Chifu Mazengo wa II amesema kuna haya ya Serikali kuanza upya kutilia mkazo kwa vitendo maswala yote yanayohusu utalii na uhifadhi na kuweka kumbukumbu kwa vizazi vijavyo.

Amesema Mkoa wa Dodoma una vivutio vingi vya kihistoria ambayo vikiwekewa alama vitakuwa na hadhi na kuvutia Utalii.

"Vivutio vya asili Dodoma ni vingi  lakini utambuzi wake imesahaulika mfano hapa Kikuyu mbali na kuwepo kwa eneo la tembo,ukiingia ndani ya chuo kikuu cha St.Jonh  kuna mti mkubwa uliotumika kunyongea wahalifu kipindi Cha utumwa lakini ukiwauliza wanaosoma pale hawajui chochote kuhusu mti huo,"amesema


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post