WANANCHI MWAMANYUDA WALIA CHANGAMOTO UHABA WA WATAALAMU WA AFYAMtaalamu wa afya katika zahanati ya kijiji cha Mwamanyuda Sophia Tanganyika.Na Halima Khoya,Shinyanga.

Wananchi wa kijiji cha Mwamanyuda Kata ya Imesela Wilaya ya Shinyanga wameiomba serikali kuwaongezea wataalamu wa afya katika zahanati ya kijiji ili kuondokana na adha ya kukosa huduma kwa wakati.


Wakizungumza wakati wa ziara ya kamati ya chama cha Mapinduzi(CCM) Kata ya Imesela baadhi ya wananchi wamesema kumekuwa na changamoto ya kuchelewa kuhudumiwa na wahudumu licha ya kuwepo kwa huduma nzuri lakini wameomba kuongezewa wataalamu hao.


Miongoni mwa wananchi hao akiwemo Sophia Ntemanya na Sultan Nshishi wameeleza uwepo wa uhitaji wa kuongezewa wataalamu wa afya kwani kumekuwa na mizunguko mingi inapotokea mgonjwa anahitaji kupatiwa huduma na mjamzito anatakiwa kuzalishwa hivyo wahudumu wawili hawatoshi.


"Yaani inapotokea nimefika zahanati nataka kuhudumiwa halafu wakati huo huo nesi anataka akamzalishe mtu mwingine,hivyo unakuta mtu unachelewa kupata matibabu kwa haraka,tunaiomba serikali iliangalie hilo na kitu saidia kutuletea wataalamu zaidi", amesema Ntemanya.


Kwa upande wake nesi anayefanya kazi katika zahanati hiyo,Sophia Tanganyika amesema kuwa wanafanya kazi kwa muda mrefu kwa sababu ya uchache wao hali iliyosababisha kufanya kazi bila kupata muda wa mapumziko sambamba na kuomba kupelekewa mganga wa zahanati hiyo.


Diwani wa Kata ya Imesela, Seth Msangwa,amesema kuwa amezungumza na ofisi ya Mkurugenzi wa halmashauri juu ya changamoto hiyo na kuahidi kulifanyia kazi ikiwa ni pamoja na kuwaongezea wataalamu wa afya katika zahanati hiyo.


"Nilimshirikisha Mganga mfawidhi alisisitiza atalifanyia kazi,kwa haraka haraka ni vigumu sana kupata mfanyakazi,ndani ya Halmashauri yetu kuna hospitali zina uchache wa wataalamu wa afya hivyo tuwe na subra huku tukisubiria hatua zitakazochukuliwa",amesema Msangwa.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post