DC SAMIZI AWEKA JIWE LA MSINGI MRADI WA MAJI KATA YA KIZUMBI, ATAKA WANANCHI WAVUTE MAJI NDANI

Mkuu wa wilaya ya Shinyanga  Mhe. Johari Samizi akiwa kwenye gati la maji Kitongoji cha Bugayambelele kata ya Kizumbi manispaa ya Shinyanga

Na MWANDISHI WETU - MALUNDE 1 BLOG

MKUU wa wilaya ya Shinyanga  Mhe. Johari Samizi ameweka jiwe la msingi kwenye mradi maji  katika Kitongoji cha Bugayambelele kata ya Kizumbi manispaa ya Shinyanga unaotekelezwa na Wakala wa Majisafi na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) uliogharimu kiasi cha shilingi milioni 149 utakaohudumia wakazi zaidi ya elfu 10 waliopo ndani ya kitongoji hicho na maeneo jirani.

Zoezi hilo la uwekaji wa jiwe la msingi limefanyika leo Machi 31, 2023.

Akisoma taarifa ya ujenzi wa mradi huo meneja wa Wakala wa Majisafi na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) wilayani Shinyanga Mhandisi Emmael Mkopi amesema ujenzi wa mradi wa gati la maji katika kitongoji cha Bugayambelele ulianza Februari 1,2022 hadi Juni 30,2022 ulipokamilika, uliogharimu kiasi cha shilingi milioni 149 ukihusisha ununuzi wa vifaa na ulazaji wa mabonba hadi kwenye mradi huo.

Diwani wa kata ya Kizumbi Reuben Kitinya ameishukuru serikali ya awamu ya sita kupitia Wakala wa Majisafi na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) wilayani Shinyanga kwa kuendelea kutekeleza miradi ya maji vijijini na kupunguza adha ya upatikanaji wa maji kwa wananchi.

“Mpaka sasa kati ya vitongoji 17 vilivyopo ndani ya kata ya Kizumbi kuna vitongoji 3 tu bado havijafikiwa na huduma hii ya maji ikiwemo kitongoji cha Relini, kukamilika kwa gati hili la maji kwenye eneo hili itakwenda kuondoa changamoto ya upatikanaji wa maji iliyokuwa ikisumbua kwa muda mrefu,ni dhahili tunaona namna serikali ya chama cha mapinduzi inavyotekeleza ilani ya chama chake”, amesema diwani Kitinya.

Akizungumza mara baada ya kuzindua mradi huo mkuu wa wilaya ya Shinyanga Johari Samizi amesema lengo la serikali ya awamu ya sita ni kuhakikisha inamtua ndoo mama kichwani kwa kuhakikisha inaondoa changamoto ya upatikanaji wa huduma ya maji kwenye maeneo mbalimbali hususani maeneo ya vijijini.

“Leo hii wakazi wa kitongoji cha Bugayambelele na maeneo jirani tumeshuhudia namna serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan inavyoendelea kuhakikisha suala la upatikanaji wa maji kuwa si changamoto ndani ya maeneo mbalimbali hivyo basi ni wajibu wa kila mmoja kuiunga mkono serikali kwa kuwa mlinzi wa miundombinu hii inayojengwa ili iweze kudumu kwa muda mrefu na kuwanufaisha vizazi na vizazi ndani ya eneo hili”,amesema.

“Niwaombe wakazi wa katongoji cha Bugayambelele tutumie fursa hii kuvuta maji kwenye nyumba zetu kwa kufanya hivyo itapunguza msongamano wa watu kwenye gati hili la maji na kurahisisha upatikanaji wa maji kwenye kila kaya”, ameongeza Samizi.

Aidha mkuu wa wilaya ametembelea miradi mbalimbali inayotekelezwa na Wakala wa Majisafi na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) wilayani Shinyanga ikiwemo mradi wa tanki la maji uliopo kijiji cha Ishinabulandi kata ya Samuye pamoja na tenki la maji katika kijiji cha Mwamala ambapo mpaka sasa miradi hiyo imefikia asilimia 70 ya utekelezaji.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Johari Samizi akizungumza na wananchi kwenye mradi wa ujenzi wa Tenki la maji lililopo kijiji cha Ishinabulandi kata ya Samuye.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Johari Samizi akimtwisha ndoo ya maji mmoja wa wakazi wa kitongoji cha Bugayambelele.
Baadhi ya wakazi wa kitongoji cha Bugayambelele kata ya Kizumbi halmashauri ya Shinyanga waliojitokeza kwenye zoezi la uwekaji wa jiwe la msingi kwenye mradi wa maji.
Meneja wa Wakala wa Majisafi na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) mkoa wa Shinyanga Mhandisi Julieth Payovela akizungumza na wakazi wa kitongoji cha Bugayambelele kata ya Kizumbi.
Mradi wa Tenki la maji katika kijiji cha Ishinabulandi kata ya Samuye.
Mhandisi Emmael Mkopi kutoka Wakala wa Majisafi na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) wilayani Shinyanga akisoma taarifa ya ujenzi wa mradi wa gati la maji katika kitongoji cha Bugayambelele, manispaa ya Shinyanga.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Johari Samizi akikabidhi hati ya makabidhiano ya mradi wa gati la maji kitongoji cha Bugayambelele kwa Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa Mazingira Shinyanga (SHUWASA) Mhandisi Yusuph Katopola.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post