KAMATI YA SIASA CCM IMESELA YAFANYA ZIARA ,YAHIMIZA WAZAZI KUCHANGIA MADAWATI..."WATOTO WANAKAA CHINI"

Na Halima Khoya, Shinyanga.


Kamati ya siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Imesela Wilaya ya Shinyanga imefanya ziara ya siku tatu kwa ajili ya kutembelea miradi ya maendeleo ikiwa ni hatua ya utekelezaji wa ilani ya Chama hicho ili kutatua changamoto zilizopo katika miradi hiyo.


Ziara hiyo imeanza Machi 6, 2023 ambapo wametembelea miradi ya elimu katika shule ya msingi Maskati na shule ya sekondari Imesela na kujadili changamoto zinazowakabili wanafunzi na utatuzi wake.


Akizungumza wakati wa kufungua kikao cha kamati hiyo kilichofanyika katika shule ya Msingi Maskati, Katibu wa CCM Kata Richard Nyanda amesema malengo ya kufanya ziara hiyo ni kutembelea miradi na taasisi zote zilizopo katika Kata hiyo ili kubaini changamoto na jinsi ya kuzitatua.


Akisoma Taarifa ya shule mkuu wa shule ya Msingi Maskati,Peter Chono Dalali amesema mwaka 2021 walisajili wanafunzi 34 waliofaulu 25 na waliofeli 9 ambayo ni sawa na 73.53%, 2022 waliosajili wanafunzi 27 waliofaulu 21 waliofeli 6 sawa na 77.78% ambapo jumla kwa miaka mitatu ilikuwa na wanafunzi 106 waliofaulu 75 na waliofeli 31 sawa na 70.75% na kufanikiwa kufaulisha wanafunzi kwa kiasi kikubwa.


Dalali amebainisha kuwa katika shule hiyo imefanikiwa kuanzisha miradi miwili, ujenzi wa nyumba ya mwalimu ambapo wanamshukuru Mbunge wa Jimbo la Solwa Mhe. Ahmed Salum kwa kutimiza ahadi yake ya kutoa mifuko 200 ya saruji pamoja na ufugaji wa mbuzi ambapo wana mbuzi 13.


Hata hivyo Dalali ameeleza juu ya changamoto ya uchache wa madawati 50 ambayo yanasababisha baadhi ya wanafunzi kukaa chini hali inayosababisha wanafunzi wengi kukata tamaa na wengine kuacha shule.


"Shule ya msingi Maskati ina jumla ya madarasa 6, ofisi 3 na matundu ya vyoo 8 ambapo moja linatumiwa na walimu, thamani tuna Madawati 65 meza 9,vitu 9, kabati 1,shubaka 3,nyumba moja ya mwalimu,kuna baadhi ya wanafunzi wanakaa chini kwani inawafanya wanafunzi wengine kukata tamaa,pia kuna upungufu wa vyumba vya walimu baada ya baadhi ya nyumba kupitiwa na mradi wa reli ya kisasa, tunapungukiwa na madarasa mawili", amesema Dalali.


Mwenyekiti wa CCM Kata ya Imesela, Sebastian Mwigulu Katambi,amesema kuwa utaratibu wa kuchangia madawati ushirikishwe kwa wazazi kwaajili kuchangia haraka na kuondokana na changamoto ya kukaa chini kwa baadhi ya wanafunzi.


Monica Mshinga na Elia Emannuel ni baadhi ya wanafunzi wanaosoma katika shule hiyo ambao wameeleza uhaba wa madawati unavyopelea kufeli na hata kukosa usikizi mzuri wakiwa katika masomo yao sambamba na kukatishwa tamaa hali inayosababisha kuwepo kwa wanafunzi wasiojua kusoma na kuandika.


Kwa upande wake Mwenyekiti wa kijiji cha Maskati,Robert Ngusa amesema kuwa awali aliitisha mkutano wa hadhara kwaajili ya kuchangia fedha za ukarabati wa madawati hayo ambapo hawakukubaliana kiasi cha kuchangia na baada ya kikao hicho wamekubaliana kuchangia elfu tatu kwa kila kaya.


Seth Msangwa ni Diwani wa Kata ya Imesela ambaye pia ni mjumbe wa kamati ya siasa amesema kuwa hali ya watoto inasikitisha baada ya kujionea baadhi ya wanafunzi wanakaa chini ambapo baada ya kuguswa na changamoto hiyo amechangia fedha kwa ajili ya ukarabati wa madawati hayo.


"Niliongea na Injinia wa ujenzi akasema hizi fedha zinatoka kwa mlolongo kwamba kutoka kwenye wizara ya ujenzi ziende kwenye wizara ya ardhi kisha ziende TAMISEMI ndipo Halmashauri wailetee Taasisi husika,tuliona watujengee kwa maana thamani ya majengo ya vyumba vya walimu vinaweza kuwa na thamani kubwa,vitu ambavyo tuliwaambia watuletee fedha ni kama ardhi na miti",amesema Msangwa.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post