SERIKALI YAAHIDI KUTATUA CHANGAMOTO SEKTA BINAFSI


Na Georgina Misama – MAELEZO.

Serikali kupitia Wizara ya Uwekezaji Viwanda na Biashara imeahidi kushirikiana na Sekta Binafsi katika kutatua changamoto zinazoikabili sekta hiyo; katika kikao cha majadiliano kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi kilichofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Julius Nyerere (JNICC), Jijini Dar es salaam.

Akiongea katika mkutano huo, Waziri wa Uwekezaji Viwanda na Biashara Dkt. Ashatu Kijaji alisema Serikali imeamua kuboresha mazingira ya Sekta binafsi ili kukuza mchango wake katika pato la taifa na kwamba ni wakati sasa wa wadau wote wa Sekta binafsi kutoa ushirikiano kwa kuwa wawazi, waadilifu, wakweli, wawajibikaji na wazalendo hasa wanapoombwa taarifa na Serikali.

“Kutokana na majadiliano yetu ya hapa leo, sote tunakiri uwekezaji, viwanda na biashara ndio msingi wa maendeleo wa taifa lolote Duniani hivyo ni muhimu tukaendelea kuimarisha, kama waziri mwenye dhamana, nawaahidi kwamba nimepokea michango yenu yote na kwamba nitaenda kusimamia na kutekeleza yote yanayowezekana na nawakaribisha milango iko wazi muda wowote, tuendelee kushirikiana,” alisema Dkt. Kijaji.

Alisema Sekta ya Umma na Sekta Binafsi zinategemeana na kwamba serikali itaanza kwa kuangalia sera, sheria, kanuni na taratibu ili kuingia kwenye utekelezaji wa azimio kubwa lililoamuliwa na kikao hicho la mpango wa kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara na uwekezaji na kuwahakikishia wajumbe namna bora ya kushughulikia mambo yote waliyoyawasilisha kupitia kamati za kitaalamu chini ya baraza la biashara (TNBC).

Akijibu baadhi ya hoja za wajumbe zilizowasilishwa katika majadiliano hayo, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha Lawrence Mafuru alisema kuna faida zaidi ya wafanyabiashara wadogo kujiweka kwenye mfumo rasmi ikiwemo kupata fursa za mikopo na kutambulika na Serikali ambapo ni rahiusi kuwekewa mazingira rafiki ya kazi zao kuliko kutojiweka wazi.

“Mnaweza mkafikiri ni faida kukwepa kodi kwa kutojiweka kwenye mifumo rasimi lakini kuna faida nyingi mnazojikosesha kwa kutojiweka wazi ikiwemo kupata mikopo kutoka kwenye taasisi za kifedha kwa ajili ya mitaji, ufahamu juu ya fursa za masoko, mitandao ya mafunzo ndani na nje ya nchi pamoja na kudorora kwa maendeleo ya nchi kwa kukwepa kulipa kodi,” alisema Mafuru.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments