MAPAMBANO DHIDI YA UKATILI KWA WATOTO NI JUKUMU LETU SOTE - SHEIKH BALILUSA


Sheikh Balilusa Bin Khamis

Na Mwandishi wetu- Shinyanga

Kaimu Mwenyekiti wa Halmashauri ya BAKWATA Mkoa wa Shinyanga Sheikh Balilusa Bin Khamis amewaagiza viongozi wa Baraza hilo ngazi za kata kuchukua hatua za haraka kukabiliana na vitendo vya udhalilishaji wanavyofanyiwa watoto.

Amesema mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia na udhalilishaji wa aina zote wanaofanyiwa watoto ni wajibu wa kila mdau kushughulikia jukumu hilo kama hatua ya kuunga mkono juhudi za serikali inayodhamiria kutokomeza matukio hayo.

Sheikh Balulisa ambaye pia ni Mwenyekiti wa kamati ya Amani Mkoa wa Shinyanga,ametoa agizo hilo wakati akizungumza na viongozi mbalimbali wa dini ya kiislamu ngazi ya kata wakiwemo Baraza la masheikh,ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kikazi.

Sheikh Balilusa amewakumbusha viongozi hao kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia miongozo na matakwa ya katiba ya BAKWATA ikiwa ni pamoja na kujenga mahusiano mema miongoni mwao, kuimarisha ushirikiano, umoja na mshikamano pamoja na kuonyesha upendo wa dhati kwa waumini wao.

Kiongozi huyo amehitimisha ziara yake ya siku mbili, iliyoanza Februari 14, kwa lengo la kutembelea na kukagua uhai wa baraza la waislamu katika wilaya ya Shinyanga ikiwa ni pamoja na kukagua miradi inayotekelezwa katika maeneo hayo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post