MADIWANI SHINYANGA DC WALIA NJAA...WAIOMBA SERIKALI KUONGEZA MAHINDI YA BEI NAFUU


Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo,Nice Munissy akizungumza kwenye baraza la Madiwani. Picha na Halima Khoya
Mwenyekiti wa halmashauri ya Shinyanga,Ngasa Mboje, akizungumza kwenye baraza la Madiwani
Madiwani wakiwa ukumbini
Madiwani wakiwa ukumbini
Madiwani wakiwa ukumbini
Madiwani wakiwa ukumbini
Madiwani wakiwa ukumbini

Na Halima Khoya, Malunde 1 blog

Madiwani wa halmashauri ya Shinyanga Mkoani Shinyanga wamemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwaletea zaidi ya Tani 226 za mahindi ya  bei nafuu kutoka Wakala wa Ghala la Hifadhi ya Chakula (NFRA) Kanda ya Shinyanga ambayo yamesambazwa kwenye baadhi ya Tarafa zenye changamoto ya uhaba wa chakula. 


Madiwani hao wametoa shukrani hizo kwenye kikao cha baraza la pili la  Madiwani lililofanyika Februari 10,2023 ambapo wamesema uhaba wa chakula ni changamoto kubwa kwa wananchi.

Hata hivyo licha ya kupokea msaada huo wa chakula cha bei nafuu bado wanaiomba serikali kuwaongezea mahindi hayo. 

Madiwani hao akiwemo Hellena  Daudi na Isack  Sengerema wamesema wananchi wanakabiliwa  na tatizo la njaa hivyo wameomba kuletewa tena msaada wa mahindi ya bei nafuu.

Awali akitoa taarifa za utendaji kazi wa Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga, Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo,Nice Munissy, amesema  Rais wa  Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa zaidi ya tani 226 za mahindi baada ya kuwa na changamoto ya uhaba wa chakula ambapo zimepelekwa kwa baadhi ya tarafa zenye uhitaji ikiwa ni pamoja na Didia, Ilola, Mwakitolyo, Lyabukande, Mwenge na Salawe na kwamba kilo moja inauzwa  shilingi 830/= ikiwa ni punguzo la shilingi 500/= kwa bei ya kawaida.

Munissy amesema kuwa kulingana na uhitaji wa mahindi katika Halmashauri yake ataandika barua kuiomba Serikali kuongeza mahindi ya bei nafuu ili kuondokana na tatizo hilo.

“Wakala wa Ghala la Hifadhi ya Chakula (NFRA) Kanda ya Shinyanga wakati wanatuletea hayo mahindi walihitaji kuwe na vituo vitatu ambavyo watahudumia vikae kitarafa, wakileta sisi ndio tunabaki navyo wenyewe, kulingana na uhitaji mkubwa wa halmashauri, ofisi yangu itaandika barua kwa NFRA kutusaidia changamoto hii”, amesema Munissy.

 Kwa upande wake Katibu Tawala Wilaya ya Shinyanga,Boniphace Chambi, amesema mahindi hayo yanatolewa na NFRA ambao wanasambaza huduma hiyo huku akiwataka wananchi hao wafike katika kata zilizofikiwa na huduma hiyo ili kununua mahindi hayo kwa bei nafuu ikiwa ni pamoja na kushukuru kwa kidogo walichopelekewa.

Mwenyekiti wa halmashauri ya Shinyanga,Ngasa Mboje, amewataka wananchi kuwapeleka watoto waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza ili kuunga jitihada za Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye ametoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu mbalimbali ya shule.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post