WAFANYABIASHRA MHUNZE WALALAMIKA MADUKA YAO KUFUNGWA KIBABE.... DED ASISITIZA NI WAJIBU KULIPA KODI

Mfano wa mlango ukiwa umefungwa

Na Sumai Salum - Kishapu
Baadhi ya wananchi na wafanyabiashara mbalimbali makao makuu ya wilaya ya Kishapu Mkoani Shinyanga (Mhunze) wameilalamikia ofisi ya mapato ya halmashauri ya wilaya ya Kishapu kwa kuwafungia biashara zao kwa madai ya kudaiwa Kodi.


Wakizungumza na waandishi wa habari mapema leo Februari 21,2023 baada ya tukio hilo kutekelezwa na maofisa biashara kwa masharti ya kutotajwa majina wala picha zao wamesema kuwa hali ya biashara kwa sasa ni ngumu jambo linalopelekea wao kushindwa kulipa kodi kwa wakati kwani fedha inayopatikana kwa faida ndogo inatumika kulisha familia.


Mmoja wa wafanyabiashara hao anayefanya kazi Stendi ya halmashauri ya wilaya iliyopo Isoso amesema kuwa hali ya biashara kwa sasa ni ngumu licha ya kuwa wao ni wazalendo kulipa kodi lakini kutokana na eneo analofanyia kazi kuwa ni stendi serikali ya halmashauri imeshindwa kusukuma magari yote kwenda stendi na badala yake wamekuwa wakivizia wateja wanaosafiri na magari ya kwenda Lalago - Meatu.


“Leo majira ya saa 4 asubuhi wamekuja maofisa biashara kutoka Halmashauri kudai Kodi, ni kweli tunadaiwa na hatujakataa kulipa lakini utaratibu ambao wamekuja nao siyo mzuri wanatumia mabavu, kitendo ambacho ni kinyume na Tamko la Rais Samia la kudai Kodi kwa ustaarabu”,amesema mmoja wa wafanyabiashara hao.


Mfanyabiashara mwingine wa duka la rejareja Mhunze senta amelaani kitendo hicho na kushauri serikali ya halmashauri kuongeza muda kidogo ili waendelee kutafuta fedha za kulipia.


"Mimi ningeshauri kama wanania ya kuendelea kukusanya mapato kulikoni nifunge na kuachana na biashara ni heri watupe muda kidogo ili tuwatafutie fedha hizo najua kodi inasaidia watoto wetu mashuleni na hata sisi akina mama hospitalini ila kwa hili la kutufungia wanatufanyia vibaya sasa hapa nikikaa nyumban nitapata wapi fedha za kuwalipa yaani halmashauri ni bora TRA wana usikivu na ukiwaeleza maafisa wake wanatufokea tu na kusema tumetumwa kutekelezwa Sheria", amesema mfanyabiashara huyo.


“Yaani wanafungia hovyo biashara harafu wanazuia usikuchukue hata hela za mauzo wala simu kama umeiacha ndani na hakuna kuzima Jokofu na wakati lina soda ndani je chupa zikipasuka itakuwaje, na wilaya hii ya Kishapu inatabia ya kudai kodi kwa mabavu tuna muomba Rais aimulike Kishapu,”ameongeza mfanyabiashara mwingine.


Hata hivyo Mkurugenzi mtendaji halmashauri ya Kishapu Bw. Emmanuel Johnson amesema kuwa hiyo inawakumbusha mfumo wa uwajibikaji kati ya halmashauri na wananchi walipa Kodi na walitakiwa kulipa Kodi muda kitambo kwani umepita zaidi ya miezi miwili sasa.


"Hakuna namna zaidi ya kulipa Kodi hatuwezi kusikiliza sababu za watu wote, ndiyo tunaamini wapo ambao wana sababu za msingi hivyo waje kwenye ofisi zetu waeleze kama zina tija tutawasikiliza na kuwasaidia otherwise walipe Kodi, kama mtu anamtaji atashindwaje kulipa Kodi?, fikiria ndugu mwandishi kama kituo tu cha afya cha Mwamalasa kinahitaji Milioni 500 tutazitoa wapi kama si kwa watu kulipa kodi wako watu wanapoteza maisha kwa kutembea umbali mrefu kufuata huduma ya afya na hatuko tayari kuendelea kupoteza watu kwa madai ya wafanyabiashara wameshindwa kulipa Kodi" ,amesema Mkurugenzi huyo wa halmashauri.


"Nimetoa maelekezo ofisi ya biashara kufunguliwa dirisha ambalo litamsikiliza kila mfanyabiashara na atajaza fomu kueleza atalipa baada ya muda gani", ameongeza Mkurugenzi.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post