GGML KUWAPATIA MAFUNZO KAZI WAHITIMU 50 WA VYUO VIKUU NCHINI

JUMLA ya wahitimu 50 wa vyuo vikuu nchini wamepata fursa ya kupata mafunzo yanayotolewa na Kampuni ya Geita Gold Mining Ltd (GGML) katika fani mbalimbali ndani ya idara za kampuni hiyo mwaka huu kwa lengo la kuwezesha wahitimu hao kupata uzoefu na kuwa na sifa za kuajirika kwenye soko la ajira.

Akizungumza mjini Geita jana katika hafla ya kuwakaribisha wahitimu hao waliogawanywa kwenye idara mbalimbali za kampuni hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa GGML, Terry Strong alisema kupitia Mpango wa Mafunzo kazini, kampuni hiyo imekuwa mdau mkubwa katika kuunga mkono mipango ya serikali ya kuimarisha uwezo wa wahitimu kuajiriwa nchini Tanzania baada ya kutekeleza mafunzo ya kazi na programu nyingine za wahitimu kwa miaka kadhaa.


GGML pia inachangia katika kukuza ujuzi nchini kwa kuwapa wahitimu fursa ya kupata uzoefu wa kazi katika nyanja mbalimbali ya ujuzi.

Mpango wa mafunzo kazini hutoa fursa kwa wahitimu wasio na ajira kupata uzoefu wa kazi ambao utakamilisha masomo yao na kuwapa uzoefu ambao unaweza kuwasaidia kukubalika katika soko la ajira.

"Programu ya mafunzo hayo inatekelezwa kwa kipindi cha miezi 12 na mwaka huu GGML imetoa nafasi za mafunzo kwa wahitimu 50 kati yao wanawake 30 na wanaume 20. Tungependa kuwatakia kila la heri wanaporipoti leo kwa idara zao tofauti,” alisema

Aidha, naye Dk. Kiva Mvungi, Meneja Mwandamizi wa Afya, Usalama, Mazingira na Mafunzo wa GGML, pia aliwapongeza wahitimu waliojiunga na GGML mwaka huu na kuwaonya kuwa makini na matapeli wa ajira.

“Jihadharini na matapeli! GGML haipokei pesa ili upate kazi au fursa nyingine yoyote ndani ya kampuni. Iwapo utaombwa pesa ili upate ofa ya kazi au unashuku jambo kama hilo, tafadhali ripoti hili mara moja kwa Idara yetu ya Usalama, Kitengo cha Upelelezi, kwa kupiga simu +255 756 808 128 / +255 28 216 01 40 Ext 1559 (viwango vinatumika), ” alionya Dk. Mvungi

Aliongeza kuwa tangu GGML ianzishwe, imekuwa ikifanya kazi kwa karibu na mamlaka za serikali za mitaa kusaidia miradi kadhaa ya jamii katika mkoa wa Geita kupitia Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi pamoja na programu za Kitaifa.


“Novemba 2022, GGML ilitambuliwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kama mlipakodi anayekidhi viwango vya ubora katika tasnia ya madini nchini wakati Desemba 2022, Kampuni ilinyakua tuzo mbili katika Tuzo za Chama cha Waajiri Tanzania (ATE): nafasi ya kwanza katika utekelezaji sera ya Wajibu wa Kampuni kwa jamii na mshindi wa Pili miongoni mwa waajiri bora wa sekta ya binafsi,” alisema.

 
Dk. Kiva Mvungi, Meneja Mwandamizi wa Afya, Usalama, Mazingira na Mafunzo wa GGML akizungumza na wahitimu hao ambao wamegawanywa katika idara mbalimbali za GGML kwa lengo la kuwapatia mafunzo kazini yatakayofanyika kwa muda wa miezi 12.

Mkurugenzi mkuu wa GGML, Terry Strong (kushoto) na Dk. Kiva Mvungi, Meneja Mwandamizi wa Afya, Usalama, Mazingira na Mafunzo wa GGML (kulia) wakizungumza na wahitimu hao ambao wamegawanywa katika idara mbalimbali za GGML kwa lengo la kuwapatia mafunzo kazini yatakayofanyika kwa muda wa miezi 12.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments