ENEO LA KITARAKA KUTUMIKA KIMKAKATI KUZALISHA MIFUGO KIBIASHARA


*****************************

Na Mbaraka Kambona, Singida

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega (Mb) amesema kuwa Serikali imedhamiria kulitumia eneo la kupumzishia mifugo la Kitaraka lililopo wilayani Manyoni, Singida liweze kutumiwa na vijana watakao hitimu mafunzo katika vituo atamizi kwa ajili ya kufanya shughuli za uzalishaji wa mifugo kibiashara ili kukuza uchumi wao na Taifa kwa ujumla.

Mhe. Ulega alibainisha hayo wakati wa kikao baina yake na Mkuu wa Mkoa wa Singida, Mhe. Peter Serukamba (kushoto) alipokutana nae katika ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Manyoni, mkoani Singida Januari 30, 2023.

Wakati wa mazungumzo yao, Mhe. Ulega alimueleza Mkuu wa Mkoa huyo kuwa lengo la ziara yake ni kujadiliana nae kuhusu dhamira ya Serikali ya kutaka kulitumia eneo la kitaraka kwa ajili ya kufanya shughuli za uzalishaji wa mifugo ili kuwawezesha vijana kujipatia ajira lakini pia kuzalisha malighafi ya uhakika kwa ajili ya viwanda vya nyama na kuifanya sekta ya mifugo kuchangia ipasavyo katika pato la taifa na la mtu mmoja mmoja.

Alisema kuwa kupitia programu ya vituo atamizi iliyoanzishwa na serikali kwa ajili ya kuwafundisha vijana ufugaji wa kisasa, Serikali imetenga jumla ya Shilingi Bilioni 19 kwa ajili ya kuwawezesha vijana kufuga kibiashara kwa ajili ya kuuza ndani na nje ya nchi.

“Progaramu hii ya vituo atamizi ni ya miaka 3(2022/23-2024/25) na hizi bilioni 19 zinatolewa na wadau mbalimbali ambapo serikali inatoa bilioni 6.3, na bilioni 12.6 zitachangiwa na wadau wengine kutoka sekta binafsi”,alisema Ulega

Aliongeza kwa kusema kuwa mpango huo wa kutumia eneo la Kitaraka unatarajiwa kuzalisha robota 500,000 za malisho ya mifugo na kunenepesha ng’ombe 8000 kwa wakati mmoja.

Aidha, alifafanua kuwa eneo hilo la Kitaraka limekaa kimkakati kwa ajili ya unenepeshaji wa mifugo kwasababu ndani ya eneo hilo kuna kituo cha treni ya mwendokasi (SGR) hivyo itarahisisha usafirishaji wa malighafi kutoka hapo kwenda maeneo mengine ya soko. Aidha, Naibu Waziri alimuomba Mkuu wa Mkoa, uongozi wa halmashauri, na wananchi wa Singida kwa ujumla kuhakikisha wanatoa ushirikiano wa dhati katika kufanikisha adhma ya serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kukuza ajira kwa vijana kupitia sekta ya mifugo.

“Serikali ya Mhe Rais, Dkt. Samia imejielekeza ipasavyo ktk kutumia fursa za sekta za Mifugo,uvuvi na kilimo katika kuajiri Vijana na kuongeza uzalishaji nchini hivyo naomba mtoe ushirikiano wa kutosha ili adhma hii iweze kutimia kama ilivyokusudiwa”, alifafanua Mhe. Ulega

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments