MAJESHI : VIONGOZI WA CCM NI LAZIMA WAWE WAKOMAVU WA SIASA...BADO KUNA NONGWA NAFASI YA UBUNGE, SERIKALI ZA MITAA

 

Katibu wa CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini, Ally Majeshi akizungumza kwenye mkutano wa hadhara katika kata ya Masekelo Manispaa ya Shinyanga.

Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog

Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Shinyanga Mjini, Ally Majeshi amewataka viongozi wa Chama cha Mapinduzi na wale waliopewa ridhaa kwa tiketi ya CCM ni lazima wawe wakomavu wa siasa, mtu asitumie cheo chake kutengeneza maneno maneno na malumbano ndani ya chama hicho.


Majeshi ametoa kauli hiyo leo Jumapili Januari 29,2023 kwenye mkutano wa hadhara katika kata ya Masekelo Manispaa ya Shinyanga wakati Mjini imeadhimisha Miaka 46 ya kuzaliwa kwa Chama cha Mapinduzi (CCM)


“Tunapotimiza miaka 46 bado kuna maeneo na watu, ndani ya CCM kuna watu wanadhani chama hiki kina miaka minane hawa wanatakiwa wapimwe na madaktari. Bado ndani ya CCM tuna nongwa za uchaguzi. Tuna nongwa za uchaguzi wa serikali za mitaa 2019, kura za maoni kuwapata wenyeviti wa serikali za mitaa kwenye mikutano mikuu yao ya chama ya matawi”,amesema Majeshi.

“Wanaojaliwa kuteuliwa kupata nafasi za kupeperusha bendera wanafikiri wamepewa hatimiliki ya hizo nafasi walizopewa au wao ndiyo watu sahihi ndani ya chama jambo ambalo siyo sahihi kabisa, waache, tuwaombe wanachama wetu, viongozi wetu nongwa za uchaguzi ziishe.

Lakini mwenyekiti tulivyotoka mwaka 2019 tukaenda 2020 nongwa za ubunge zipo, tunazo nongwa kwenye hiyo nafasi ya Ubunge. Unapopewa nafasi au ridhaa ndani ya chama ni umepewa nafasi na ridhaa kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi, hujamilikishwa chama, maana yake nini Mwenyekiti? Viongozi wetu waliopewa dhamana wasifanye kazi ya kukigawa chama kwa sababu ya kwamba, kwa kuwa wao wana nafasi basi wale ambao waliomba nao ridhaa hawana thamani na heshima na hadhi ndani ya chama, jambo hili mwenyekiti siyo sahihi”,ameeleza Majeshi.

“Mwenyekiti nisipoyasema haya tutakuwa tunaendelea kuongoza chama chenye mabaka mabaka na makovu, maajali na matatizo yasiyokuwa na sababu.  Mwaka wa 2022 tumetoka kwenye uchaguzi wa chama na bahati nzuri uchaguzi huo wa 2022 mimi nilikuwa mkurugenzi wa uchaguzi ndani ya chama nawafahamu wanachama na viongozi wanaoendeleza nongwa za uchaguzi, chama hiki chetu wote sisi, aliyepewa nafasi ni chama chake na aliyekosa nafasi naye ni chama chake”,ameongeza Majeshi.

Majeshi amewataka wanachama na viongozi wenye tabia ya kutaka kuivuruga CCM waache.

“Mhe. Mwenyekiti watu waacha tabia za kukivuruga chama kwa sababu ya tafsiri potovu ambazo anakuwa nazo yeye mwenyewe mtu binafsi, haiwezekani mwenyekiti leo tukawa na kiongozi mwenzetu ana jambo lake halafu wanaCCM wakaenda kumsaidia, halafu kiongozi wa chama kama mimi Majeshi nikalalamika kwanini wanachama wameenda kwake, hii siyo sahihi”,amesema Majeshi.

Soma pia:

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments