CCM YAJIGAMBA HAIOGOPI MIKUTANO YA HADHARA "TWENDENI SASA TUKASHINDANE KWA HOJA"


 
HATUA ya Rais Dk Samia Suluhu Hassan kuondoa zuio la mikutano ya hadhara kwa vyama vya siasa, imepongezwa na Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Iringa kilichosema haiwapi hofu yoyote ya ushindani wa kisiasa dhidi ya vyama vingine vya siasa.  
 
Akizungumza na wanahabari mjini Iringa leo, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Iringa Daudi Yasin amesema; “Uamuzi huu wa Rais utatuimarisha zaidi na kutuweka jirani na wananchi tunapotaka kuwafafanulia utekelezaji wa Ilani na ahadi zetu mbalimbali.”

Katika mkutano huo na wanahabari uliohusisha viongozi wa chama hicho wa wilaya zote na Chifu wa Wahehe Adam Abdu Sapi Mkwawa, Yasin alisema kilichofanywa na Rais Dk Samia kinaonesha jinsi alivyo na nia njema kukuza demokrasia na kuongeza umoja, upendo na mshikamano miongoni mwa Watanzania.

“Uamuzi huo unatuweka katika mazingira ya kuendelea kuaminiwa zaidi na wananchi na ni tiketi nzuri kwetu ya kujipatia ushindi wa kishindo katika chaguzi zijazo za serikali za mitaa na Uchaguzi Mkuu,” alisema.

Yasin aliwataka wanaCCM wote kuupokea uamuzi wa Rais kwa mikono miwili akisema hauwezi kukiathiri chama chao na imani waliyonayo kwa wananchi katika majimbo yote saba ya uchaguzi katika mkoa huo.

Mwenyekiti wa CCM Manispaa ya Iringa, Said Rubeya aliongeza kwa kuwaondoa hofu wapiga kura wa jimbo la Iringa Mjini akisema utekelezaji mzuri wa Ilani na kazi ya siasa watakayoendelea kuifanya itawapa ushindi mkubwa zaidi katika chaguzi zijazo.

“Baada ya uamuzi huu, tunajua macho na masikio yataelekezwa mjini Iringa ambako huko nyuma kuliwahi kuongozwa na upinzani. Niwahakikishie jimbo hili na halmashauri hii haviwezi kurudi huko,” alisema.

Nao viongozi wa chama hicho wa Wilaya ya Mufindi, Kilolo na Iringa Vijijini waliupongeza uamuzi huo wa Rais wakisema wataitumia fursa hiyo kufanya siasa za kistaarabu na kuendelea kuleta maendeleo kwa wananchi.

Mwenyekiti wa CCM Kilolo, John Kitive alisema Rais Samia anastahili kupongezwa kwa moyo wake wa kishujaa wa kurudisha kazi za kisiasa kwa vyama vyote vya siasa.

“Twendeni sasa tukashindane kwa hoja, sio matusi, vitisho au vihoja. Tukawaeleze wananchi nini kimefanywa na serikali yao na nini kifanyike ili kusukuma zaidi maendeleo,” alisema.

Wakati huo huo, Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Iringa amesema chama chao kinao chawa wengi na wengine wengi wanatarajiwa kuongezeka ili kuunga mkono yale yote mazuri yanayofanywa na serikali yao.

“Wanaofikiri chawa ni watu wabaya tunawaomba waondokane na mtizamo huo. Chawa tunaokereketwa na chama chetu, maendeleo ya nchi, utu na heshima ya viongozi wetu tupo na tunatarajia kuongezeka zaidi baada ya Rais kuruhusu mikutano hii ya kisiasa,” alisema Yasin. 
 
SOMA HAPA ZAIDI CHANZO HABARI LEO

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments