MUME MBARONI TUHUMA ZA KUMUUA MKEWE KWA KUMCHOMA KISU MSHIKAMANO SHINYANGA MJINI

Joyce Masanja enzi  za uhai wake

Na Mapuli Misalaba, Shinyanga

Mwanaume mmoja mkazi wa mtaa wa Kalonga kata ya Ngokolo katika Manispaa ya Shinyanga anashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za mauaji ya Mke wake Joyce Masanja kwa kumchoma kisu.

Tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia leo Jumamosi Januari 14,2023 ambapo mwili wa mwanamke huyo umekutwa ukiwa umetelekezwa jirani na msikiti uliopo Mtaa wa Kalonga kata ya Ngokolo.

Misalaba Blog imefika katika eneo la tukio na kuzungumza na wakazi wa mtaa wa Kalonga jina maarufu Mshikamano ambao wameeleza kuwa tukio hilo limetokea majira ya saa sita usiku ambapo baadhi yao wamesikia sauti ya marehemu huyo akikimbizwa na watu wawili huku akipiga kelele.

Majirani wamesema baada ya kusikia kelele hizo kwa muda mfupi umeme ulikatika na kwamba hawakusikia tena kelele ndiyo asubuhi walimkuta Joyce Masanja amefariki dunia pembezoni mwa barabara jirani na msikiti.

Baadhi ya wananchi waliofika kwenye tukio hilo wameeleza kuwa wamekuta mwanamke huyo amefariki Dunia huku akiwa amechomwa kisu sehemu mbalimbali za mwili wake ikiwepo sehemu ya shingo, kwenye ubavu pamoja na sehemu ya mapaja yake.

Wameeleza kuwa wamesikitishwa na tukio hilo ambapo wameilalamikia serikali ya mtaa huo kuwa wanatoa mchango wa fedha kila mwezi kwa ajili ya ulinzi shirikishi na kwamba ulinzi huo haufanyiki ipasavyo huku wakiliomba jeshi la polisi kufanya uchunguzi ili kubaini chanzo cha mauaji ya Mwanamke huyo Joyce Masanja.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Mtaa wa Kalonga Bwana Victor Ochieng ameeleza kuwa amepokea taarifa za tukio hilo majira ya saa moja asubuhi ambapo alichukua hatua za kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi,ambapo pia ametoa rai kwa jamii kuepuka tabia ya kujichukulia sheria mkononi


Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga Kamishina Msaidizi wa polisi Janeth Magomi amethibitisha kutokea kwa tukio hilo ambapo ameeleza taarifa za awali zinaonesha chanzo ni wivu wa kimapenzi baina ya Mume na Mke,na kwamba jeshi hilo linamshikilia mwanaume huyo kwa ajili ya uchunguzi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments