WATEMBEA ZAIDI YA KILOMITA 15 KUFUATA HUDUMA ZA AFYA ..."WAJAWAZITO WAJIFUNGULIA NJIANI"


Jengo la Zahanati ya Nyida Halmashauri ya Shinyanga ambalo limejengwa kwa nguvu za wananchi na halijaanza kutumika
Mkazi wa Kata ya Nyida akizungumza na mwandishi wa habari
Afisa mtendaji Kata ya Nyida Daudi Lazaro akizungumza na mwandishi wa habari
****
Na Mwamvita Issa - Shinyanga

Umbali wa huduma za afya maeneo ya vijijini bado ni changamoto kubwa licha ya jitihada kubwa zinazofanywa na serikali kuhakikisha wananchi wake wanapata huduma karibu lakini mahitaji ni makubwa ambayo yanahitaji nguvu ya wadau, wananchi na serikali kuweza kuwasaidia wananchi.


Kutokana na umbali wa huduma wananchi wamekuwa wakilazimika kutembea na wengine kusafiri umbali mrefu kufuata huduma za afya zaidi ya kilomita 15,jambo ambalo limekuwa likisababisha baadhi ya akinamama wajawazito kujifungulia njiani na wagonjwa wengine kupoteza maisha.


Katika kuhakikisha changamoto hiyo inakwisha serikali inapaswa kusogeza huduma karibu na wananchi hususani huduma za afya,kwa mujibu wa sera ya afya ya June mwaka 2007 ambayo inaeleza kila kijiji kuwa na zahanati na kila kata kuwa na kituo cha afya lakini utekelezaji wake bado haujafanikiwa kuweza kuondoa adha hiyo kwa wananchi.


Changamoto hizo za afya zinabainishwa na wakazi wa Vijiji vya Nduguti, Igembya na Nyida Halmashauri ya Shinyanga ambao wametoa kilio chao kwa serikali kuwatatulia changamoto ya kusafiri zaidi ya kilomita 15 kwenda zahanati ya Kijiji cha Nyashimbi kilichopo kijiji Kata ya Puni, kituo cha afya Tinde na Bugisi.


Wananchi wanasema kukosekana huduma za afya karibu inawalazimu kutembea umbali wa zaidi ya kilomita 15 kufuata huduma za matibabu kata jirani ya Puni na maeneo mengine huku baadhi ya wajawazito wakijifungulia njiani na kuhatarisha maisha ya mama na mtoto.


Kufuatia changamoto hiyo,wananchi wa Kijiji cha Nyida wameamuwa kuchangia nguvu kazi kwa kuanzisha ujenzi wa jengo la zahanati ambalo liko hatua za mwisho kukamilika ambalo litasaidia kuwaondolea adha wananchi kufuata huduma umbali mrefu.


“Tunapata tabu sana maana hakuna huduma za afya karibu tunapohitaji kupata matibabu tunasafiri umbali mrefu zaidi ya kilomita 15 na vijiji vingine vilivyopo karibu umbali ni wastani wa kilomita10,tunapata taabu sana tunaiomba serikali itusaidie kutusogezea huduma karibu”, anasema Devota David mkazi wa Kijiji cha Nyida.


Anasema kutoka Kijiji cha Nyashimbi hadi kituo cha kupata huduma ni umbali mrefu na kusababisha wakati mwingine wakinamama wajawazito wanazalia njiani hivyo kuhatarisha maisha ya mama na mtoto,pia wanapohitaji kupeleka watoto chanjo inakuwa changamoto na na wengine wanashindwa kupata huduma.


Anabainisha kuwa unaweza kupata mgonjwa usiku ama mama mjamzito anaumwa uchungu anatakiwa kwenda kujifungua sehemu ya kupata huduma ni mpaka Tinde, Bugisi na Nyashimbi na usafiri unaotumika ni pikipiki tunatozwa fedha nyingi tunaiomba serikali itusogezee huduma.


Katika kukabiliana na changamoto hiyo wananchi wamechangia nguvu kazi kwa kujenga jengo la zahanati ili kuondoa changamoto ya kufuata umbali mrefu huduma za matibabu ambapo Afisa mtendaji Kata ya Nyida Daudi Lazaro, anaeleza kuwa kilio kikubwa cha wananchi ni kupata huduma za afya karibu.


Afisa mtendaji anasema, akina mama wajawazito na watoto chini ya umri wa miaka mitano wanapata changamoto sana hususani kipindi cha masika mvua zikiwa zinanyesha wanashindwa kwenda kliniki na kupata huduma zingine za kitaalamu jambo ambalo ni hatari kwa afya ya mama na mtoto.


Kufuatia hali hiyo kwa kushirikiana na wananchi wa Kijiji cha Nyida wameamuwa kuchangia nguvu zao kwa kujenga jingo la zahanati ambapo pia halmashauri iliongeza nguvu na liko hatua za mwisho kukamilisha ili changamoto hiyo wanaondokane nayo wananchi wa Kijiji cha Nyida lakini pia vijiji vingine vya Kata hii bado navyo havina zahanati.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments