MENEJIMENTI YA TAWA YATAKIWA KUFANYA KAZI KWA USHIRIKIANO


**********************

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) ameitaka menejimenti Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) ifanye kazi kwa ushirikiano ili kuiwezesha taasisi hiyo kutimiza malengo yaliyowekwa.

Mhe. Mary Masanja ametoa kauli hiyo leo jijini Mwanza mara baada ya kuitembelea menejimenti ya TAWA inayoendelea na mafunzo ya uongozi katika Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori Pasiansi.

Amewaeleza kuwa utendaji kazi wenye kuzingatia ushirikiano na Upendo ni nguzo muhimu itakayowawezesha kurekebishana na kukosoana kiutendaji kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa.

Aidha, amesisitiza kuwa ni vyema menejimenti hiyo ikajiwekea utaratibu wa kujadili changamoto mbalimbali pamoja ili iweze kufika mbali kiutendaji.

"Mwenzako anapokutana na changamoto yoyote ichukulie kama ni yako. Tunahitaji tufanikiwe kwa kutatua changamoto zinazotukabili kwa pamoja " amesisitiza Mhe. Masanja.

Mafunzo hayo yenye lengo la kuwajengea uwezo viongozi katika usimamizi wa masuala mbalimbali yakiwemo ya rasilimali watu, fedha na taratibu za manunuzi yametolewa kwa Manaibu Kamishna, Makamanda wa Kanda, Makamishna Wasaidizi Wandamizi na Makamishna Wasaidizi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post