KUONGEA KIZUNGU SI USTAARABU, USTAARABU NI KUPELEKA KISWAHILI KILELENI

  Na Dotto Kwilasa, DODOMA 

KUTOKANA na harakati za kukuza lugha ya Kiswahili duniani,takribani watu milioni 250 wanatajwa kuzungumza lugha hiyo hali inayoimarisha mahusiano ya kidiplomasia,uchumi,
 kujenga amani, maendeleo na utangamano katika kona mbali mbali za dunia.

Hayo yameelezwa leo November 3,2022 Jijini Dodoma na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu,Sayansi na Teknolojia Prof.James Mdoe wakati akizindua sherehe za miaka 61 ya uhuru kwenye eneo la utambuzi wa lugha ya kiswahili ambayo itahusisha mashujaa wa lugha hiyo kupandisha  bango lenye ujumbe wa kiswahili kwenye kilele cha mlima Kilimanjaro.

Amesema kwa idadi hiyo inaonesha wazi ni kiasi gani kiswahili kinapendwa na kuongeza kuwa idadi kubwa ya vyuo vikuu 150 ulimwenguni vinatoa mafunzo ya lugha hiyo huku vituo vya radio na television 300 vikiwa vinarusha vipindi kwa lugha ya kiswahili.

Pamoja na hayo ameeleza kuwa Serikali ina mpango zaidi wa kuendeleza makubaliano na vyuo vingine nje ya nchi namna ya kufundisha kiswahili na kuongeza hamasa zaidi kwa watumiaji wa lugha hiyo adhimu.

Kutokana na juhudi hizo ametumia nafasi hiyo kuwataka mabalozi wanaoiwakilisha nchi sehemu mbalimbali duniani kuongeza kasi ya  kuhamasisha  zaidi matumizi ya kishwahili hali itakayosaidia lugha hiyo kutambuliwa na watu wengi zaidi.

Kwa upande wake mtaalamu wa lugha ya kiswahili na Mwandishi wa vitabu Kwa lugha hiyo mwenye asili ya Misri Mina Yasri amesema watanzania wanatakiwa kujivunia lugha yao na kuwataka kutambua kuwa uhuru wa mwafrika upo kwenye lugha yake ya asili na kusisitiza kuwa kuongea kiingereza si ustaarabu.

Mwandishi huyo ambaye pia ni mtafiti wa uzamiri na mtangazaji wa radio kwa lugha ya kiswahili ameeleza kuwa  ndiye Mwandishi wa kwanza nchini Misri kuandika kitabu cha kwanza cha maudhui ya kiswahili hivyo kuwataka watanzania kuwa na ari ya kuzungumza lugha yao ya asili bila kukuonea haya kiswahili.

Aidha Yasri ametumia nafasi hiyo kuwaomba Viongozi wa ngazi mbalimbali nchini kutumia fursa wanaposafiri kwenye mataifa mengine kukieneza kiswahili na kusisitiza kuwa uongozi bora hupendeza ikiwa kiongozi atapendelea kutumia lugha yake mama. 

Amesema ili mtu aheshimike na wengine anatakiwa kuwa na utambulisho wa pekee wa lugha ya asili na kwamba huo ndiyo ustaarabu na si vinginevyo huku alisisitiza kuwa kujua lugha ya asili ni burudani na uwekezaji na uwajibikaji .

Akieleza hali ya kiswahili Cairo-Misri eneo anakotoka Mwandishi huyo amesema lugha hiyo tayari inatambuliwa na kuenziwa na watu wengi na kwamba juhudi kidogo bado zinahitajika ili kuongeza nguvu zaidi katika kutafsiri vitabu vya kiarabu kwenda kwenye kiswahili.

"Tunahitaji zaidi kuongeza nguvu katika tafsiri za kiarabu kuwa kiswahili,tafsiri nyingi ni za kiswahili kwenda kiarabu,tunahitaji nguvu kubwa kila mmoja ajue umuhimu wa kiswahili,tunatakiwa kuunganishwa kwa lugha hii,"amesema

Naye mwanamashairi wa lugha ya kiswahili kutoka chuo cha jeshi Kunduchi  Mwanakombo Mwanakombo amekielezea kiswahili kama bidhaa inayojiuza na kuuzika duniani kote.

Amesema iwapo lugha hiyo itabidhaishwa vizuri itaendelea kusimamisha uhuru,heshima na umoja na kwamba kwa kuliona hilo lugha ya kiswahili kuadhimishwa kimataifa kila tarehe 7 Julai Kutokana na
Shirika la Umoja wa Mataifa la elimu , sayansi na utamaduni UNESCO tarehe 23 mwezi Novemba mwaka 2021 lilitangaza rasmi tarehe hiyo kila mwaka kuwa siku ya Kiswahili duniani.

Amefafanua kuwa UNESCO ilipitisha uamuzi huo huko makao makuu yake mjini Paris Ufaransa wakati wa mkutano wa nchi wanachama wa shirika hilo na kwamba azimio hilo  lilipitishwa bila kupingwa na utekelezaji wake ukaanza mwaka huu .

Maudhui ya maadhimisho ya mwaka huu ni Kiswahili kileleni yenye lengo  la kusongesha matumizi ya lugha ya kiswahili kama nguzo ya amani, na ustawi na wakati huo kuimarisha tamaduni mbalimbali za kiafrika .

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post