Na Mwandishi Wetu, Michuzi TV
OFISA Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) Nicodemus Mkama amesema Mamlaka hiyo wanaipongeza Bodi ya Wakurugenzi na Uongozi wa benki ya NBC kwa kufanikisha uuzwaji wa hatifungani ya Twiga na hatimaye leo hii kuorodheshwa katika Soko la Hisa la Dar es Salaam.
Aidha wanazishukuru taasisi na wataalam wote walioshiriki katika mchakato huo ambapo taasisi na wataalam hao ni pamoja na Bodi na Uongozi wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), Bodi na Uongozi wa Soko la Hisa la Dar Es Salaam, Mshauri kiongozi wa benki ya NBC, Tanzania Securities Company Limited na Optima Corporate Finance Limited, Mshauri wa Sheria, Lawhill & Co. Advocates, Mkaguzi na Mtoa Taarifa za Mahesabu, Deloitte & Touche.
Mkama ametoa pongezi hizo leo Desemba 20,2022 wakati wa ghafla ya kuorodheshwa kwa Hatifungani ya ya Twiga (NBC TWIGA BOND) katika Soko la Hisa la Dar es Salaam ambapo mgeni rasmi alikuwa iliyofanyika Waziri wa Fedha Dk Mwigulu Nchemba.
"Ninatambua kkazi hiyo haikuwa ndogo na rahisi lakini mmeweza kufanya kazi yenu vizuri na hivyo kufanikisha hatua hii kwa weledi na kwa ufanisi mkubwa. Kama ujuavyo mnamo Oktoba 31, 2022 Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) ilitoa idhini kwa benki ya NBC kuuza hatifungani ya Twiga yenye thamani ya Sh.bilioni 30 ikiwa ni toleo la kwanza la Programu ya hatifungani ya benki hii yaani Medium Term Note (MTN) Programme yenye jumla ya shilingi billioni 300.
"Hatifungani hii imekidhi matakwa ya Sheria ya Masoko ya Mitaji na Dhamana Sura ya 79; na Kanuni za Masoko ya Mitaji na Dhamana, Yaani “Capital Markets and Securities (Guidelines for the issuance of Corporate Bonds)”. Mauzo ya hatifungani ya Twiga yalifunguliwa Novemba 7, 2022 na kufungwa Disemba 62022.
"Ambapo kiasi cha Sh.bilioni 38.9 kimepatikana ikilinganishwa na shilingi bilioni 30 zilizotarajiwa kukusanywa, sawa na mafanikio ya asilimia 130. Mafanikio haya yametokana na imani waliyonayo wawekezaji katika masoko ya mitaji pamoja na elimu inayotolewa kwa umma na Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) kwa kushirikiana na wadau katika sekta ya fedha,"amesema Mkama.
Aidha, mafanikio hayo ni sehemu ya mazingira wezeshi yaliyotolewa na Serikali, ikiwa ni pamoja na kuondioa kodi ya zuio kwenye hatifungani za kampuni kama ilivyo kwa hatifungani za Serikali. Vile vile, imetokana na kushushwa kwa kiwango cha chini cha ushiriki katika uwekezaji kutoka Shilingi milioni moja hadi laki tano.
Ameongeza hatua hiyo ni muhimu kwani, inatoa matokeo chanya katika utekelezaji wa Mpango Mkuu wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha yaani Financial Sector Development Master Plan 2019/20 – 2029/30” wenye lengo la kuwezesha upatikanaji wa rasilimali fedha kwa ajili ya kujenga uchumi shindani kwa maendeleo ya watu.
Amesema mauzo ya hatifungani ya Twiga yamekuwa na matokeo chanya katika maendeleo ya masoko ya mitaji na Sekta ya Fedha kwa ujumla hapa nchini, ambapo asilimia 96.9 ya wawekezaji walioshiriki ni wawekezaji wadogo wadogo (Retail Investors) na asilimia 3.1 ni wawekezaji ni Kampuni na Taasisi (Institutional investors). Aidha, asilimia 100 ya wawekezaji ni wawekezaji wa ndani (Local Investors).
"Hatua hii ni muhimu kwani imewezesha utekelezaji wa Mpango Jumuishi wa Huduma za Kifedha yaani National Financial Inclusion Framework wenye lengo la kuongeza ushiriki wa wananchi kwenye sekta rasmi ya fedha ikiwa ni pamoja na masoko ya mitaji.
"Fedha zilizopatikana kupitia mauzo ya hatifungani ya Twiga zitatumika kugharamia shughuli za maendeleo ya benki ya NBC, ikiwa ni pamoja na kutoa mikopo kwa kampuni ndogo na za kati za ujasiriamali (Small and Medium Enterprises - SMEs); mikopo kwa wawekezaji wadogo wadogo (Retail Investors) yenye lengo la kukuza na kuendeleza ujasiriamali hapa nchini;
"Mikopo kwa ajili ya kuendeleza shughuli za kilimo; mikopo kwa ajili ya kuendeleza biashara zinazosimamiwa na zinazofaidisha akina mama na vijana; Hatua hii ni muhimu, kwani inatarajiwa kuwa na matokeo chanya katika ukuaji wa sekta binafsi na uchumi wa nchi kwa ujumla.Kama mnavyofahamu dhamira ya Serikali chini ya uongozi madhubuti wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ni kuhakikisha Sekta ya fedha inawezesha upatikanaji wa fedha ...
"Kwa ajili ya kutoa mikopo kwa kampuni ndogo na za kati za ujasiriamali (Small and Medium Enterprises - SMEs); mikopo kwa wawekezaji wadogo wadogo (Retail Investors) yenye lengo la kukuza na kuendeleza ujasiriamali hapa nchini.Hatua hii ni muhimu, kwani ina matokeo chanya katika ukuaji wa sekta binafsi; umma na uchumi wa nchi kwa ujumla,"amesema Mkama.
Hivyo basi, utoaji wa Hatifungani ya Twiga unachangia utekelezaji wa dhamira, malengo na azma ya Serikali ya kuweka mazingira wezeshi katika Kujenga Uchumi Shindani kwa Maendeleo ya Watu. Pamoja na mambo mengine, uorodheshwaji wa hatifungani ya Twiga katika soko la hisa unawapatia fursa wawekezaji kuuza hatifungani zao pale wanapohitaji fedha kwa ajili ya matumizi mengine.
Pia kujua thamani halisi ya hatifungani zao; na kuwapatia fursa wawekezaji wapya kununua hatifungani hizo, ambapo wawekazaji hao hupata riba kama faida itokanayo na uwekezaji huo. Aidha, uorodheshwaji wa hatifungani za kampuni unaongeza utawala bora na ufanisi katika uendeshaji wa Kampuni na kumwongezea mwekezaji wigo na fursa za uwekezaji.
Ameeleza hiyo inamsaidia mwekezaji kuwa na anuwai, jambo ambalo hupunguza athari za uwekezaji (Risk Diversification) huku akifafanua Serikali kupitia CMSA Aina jukumu la kusimamia, kuratibu na kuendeleza sekta ya masoko ya mitaji hapa nchini. Sekta hiyo ni muhimu katika upatikanaji wa mitaji ya muda mrefu kwa kampuni na husaidia umilikishaji kwa umma wa njia za uchumi, hivyo kuchangia utekelezaji wa miradi ya maendeleo na ukuaji wa uchumi wa nchi yetu.
"Kadiri Taifa letu linavyosonga mbele katika utekelezaji wa Sera ya Uchumi wa Viwanda, mahitaji ya fedha za kutekeleza miradi ya maendeleo hususani miundombinu unaongezeka. Ili kufanikisha azma hii, kunahitajika uwepo wa bidhaa nyingi katika masoko ya mitaji, ikiwa ni pamoja na hatifungani za kampuni.
"Uwepo wa bidhaa nyingi katika masoko ya mitaji unachangia utekelezaji wa Sera za Ukwasi katika Uchumi (Monetary Policy); kuongezeka kwa akiba hapa nchini; kupanuka kwa uwekezaji unaoleta ongezeko la ajira; Mapato kwa njia ya kodi kwa serikali na kuinua kipato cha watanzania kwa ujumla."
Aidha amesema Mamlaka itaendelea kutekeleza mikakati ya kujenga masoko endelevu na yenye ufanisi, ikiwa ni pamoja na namna ambayo masoko ya mitaji yanavyotumika kupata fedha za kutekeleza miradi ya maendeleo na hivyo kuwezesha kuchochea ukuaji wa uchumi wa nchi yetu.
Pia itaendelea kushirikiana na Wizara ya Fedha na Mipango katika utekelezaji wa mpango kazi wa njia mbadala za kugharamia miradi ya maendeleo yaani Alternative Project Financing (APF) Strategy wenye lengo la kuwezesha Serikali na Sekta Binafsi kugharamia miradi ya maendeleo kwa kuuza hisa kwa umma (equity financing); hatifungani (bonds); na vipande katika mifuko ya uwekezaji wa pamoja (collective investment schemes).
Mkama ametoa mwito kwa benki za biashara, benki za wananchi, Kampuni za bima, binafsi na za umma kutumia fursa zilizopo katika sekta ya masoko ya mitaji, ikiwa ni pamoja na kuuza hisa na hatifungani kwa umma na hatimaye kuorodheshwa katika soko la hisa ili kuongeza uwezo wa rasilimali fedha.Masoko ya mitaji ni muhimu katika kuchochea maendeleo ya sekta ya fedha na uchumi wa Taifa kwa ujumla.
"Benki za biashara hapa nchini kama Benki ya NMB, CRDB, DCB, Exim, Standard Chartered na benki za nje kama Benki ya Maendeleo ya Afrika Mashariki (EADB) na Benki ya Maendeleo ya Biashara Afrika (PTA-TADB) zimekuwa zikitumia masoko ya mitaji hapa nchini kuongeza rasilimali fedha, hivyo kuimarisha uwezo wa benki na taasisi hizo kutoa huduma kwa wateja katika sekta ya umma na sekta binafsi."
Ametumia nafasi hiyo kutoa rai kwa wadau wote wa masoko ya mitaji kuendelea kushirikiana na Serikali kupitia Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana katika kutekeleza mikakati ya kuendeleza masoko ya mitaji hapa nchini ikiwemo kuleta bidhaa mpya katika masoko haya ambazo zitaweza kuorodheshwa katika Soko la Hisa ili pamoja na mambo mengine kuwapatia wawekezaji taarifa mbalimbali kuhusiana na bidhaa hizo ikiwemo bei kwa namna iliyo wazi.
Akizungumza katika hafla hiyo Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), Bw.Nicodemus Mkama (pichani) pamoja na kuipongeza benki ya NBC kwa mafanikio hayo, pia aliipongeza serikali kwa kuweka mazingira wezeshi ambayo yamewavutia wawekezaji wengi zaidi kwenye hati fungani hiyo.
Awali akizungumza kwenye hafla hiyo Ofisa Mtendaji Mkuu wa DSE, Bi Mary Mniwasa (pichani) aliipongeza benki ya NBC kwa hatua hiyo muhimu huku akibainisha kuwa ushiriki wa benki hiyo katika soko hilo unaifanya DSE kufunga mwaka huu kwa kuorodhesha kwa hati fungani mbili za kampuni binafsi
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC, Theobald Sabi, Mkurugenzi wa Hazina wa Benki ya NBC, Peter Nalitolera (pichani), alisema mafanikio makubwa ambayo benki hiyo imeyapata kupitia hati fungani hiyo ni ishara kwamba wananchi wanaendelea kuiamini zaidi benki hiyo huku akiipongeza serikali kwa kuandaa mazingira wezeshi yaliyochagiza mafanikio hayo
Kamishna wa Idara ya Usimamizi wa Deni la Taifa wa Wizara ya Fedha na Mipango,Japhet Justine (katikati walioketi) sambamba na viongozi waandami wa Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) pamoja na wafanyakazi wa Benki ya NBC wakati wa hafla fupi ya uorodheshwaji wa hati fungani ya NBC ijulikanayo kama NBC Twiga Bond huo iliyofanyika jijini Dar es Salaam leo.
Kamishna wa Idara ya Usimamizi wa Deni la Taifa wa Wizara ya Fedha na Mipango,Japhet Justine (katikati walioketi) sambamba na viongozi waandami wa Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) na Benki ya NBC wakiwa kwenye picha ya pamoja na wafanyakazi wa DSE wakati wa hafla fupi ya uorodheshwaji wa hati fungani ya NBC ijulikanayo kama NBC Twiga Bond iliyofanyika jijini Dar es Salaam leo.
Kamishna wa Idara ya Usimamizi wa Deni la Taifa wa Wizara ya Fedha na Mipango,Japhet Justine (katikati) akigonga kengele kuashiria kuorodheshwa rasmi kwa hati fungani ya NBC Twiga katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) wakati wa hafla fupi ya uorodheshwji huo iliyofanyika jijini Dar es Salaam leo. Pamoja naye ni Afisa Mtendaji Mkuu wa DSE, Bi Mary Mniwasa (wa pili kulia), Mkurugenzi wa Hazina wa Benki ya NBC, Peter Nalitolera (kushoto), Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), Bw. Nicodemus Mkama (wa pili kulia) na mwakilishi wa Bodi ya benki hiyo Bw . Felix Mlaki (kulia)
Baadhi ya wageni waalikwa wakifuatilia hafla hiyo.