WAZAZI MWAMALA WAHAMASISHWA KUCHANGIA CHAKULA KWA WANAFUNZI SHULENI

Mfano wa mwanafunzi akipata chakula shuleni


Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog

Wazazi na walezi katika kata ya Mwamala Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga wamehamasishwa kuchangia chakula kwa ajili ya wanafunzi shuleni ili kuondoa utoro na kuongeza ufaulu kwenye mitihani.


Akizungumza na Malunde 1 blog hivi karibuni Afisa Mtendaji kata ya Mwamala Suzana Kayange amesema licha ya umuhimu wa chakula shuleni kwa wanafunzi lakini wazazi na walezi wamekuwa wakisuasua kuchangia chakula na kwenye baadhi ya shule chakula kinatolewa kwenye madarasa yenye mitihani tu.


“Nimekaa kwenye vikao vingi na wazazi kusisitiza chakula shuleni kwa wanafunzi kutokana na kwamba wanafunzi wakipata chakula ufaulu unakuwa mzuri lakini bado wazazi wanasuasua kuchangia chakula kwa ajili ya watoto wakiwa shuleni”,amesema Kayange.

“Tunaendelea kuhamasisha wazazi kuchangia chakula shuleni licha ya kwamba wazazi ni wabishi kutokana na kwamba hawajajua umuhimu wa chakula shuleni”,ameongeza Kayange.


Afisa Elimu Msingi Halmashauri ya Shinyanga Christina Bukoli amesema ili kuhakikisha wanafunzi wanapata chakula shuleni wameelekeza kila shule yenye mashamba ili mazao ya chakula lakini pia Maafisa watendaji wa vijiji na kata, maafisa elimu na wakuu wa shule wahamasishe wazazi na walezi kuchangia chakula kwa ajili ya wanafunzi shuleni.


Mmoja wa wazazi, Martha Tungu amesema zoezi la kuchangia chakula limekuwa likisuasua kutokana na wazazi kuwa na uelewa mdogo juu ya umuhimu wa chakula shuleni.

“Ushauri wangu wazazi tuchangie chakula ili kuinua kiwango cha ufaulu..Tuache mitazamo ya kwamba chakula kikitolewa kitaliwa na wasiohusika”,amesema Shija Kanambu mkazi wa kijiji cha Bunonga.


Nao Masesa Masele, Kang’wa Cherehani na Nyamizi Manoni wamesema kutokana na hali ngumu ya maisha wameiomba serikali itoe chakula bure shuleni.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments