HALMASHAURI YA SHINYANGA INAVYOLIPA KIPAUMBELE SUALA LA VYUMBA VYA KUJISTIRI NA TAULO ZA KIKE KWA WANAFUNZI


Mfano wa taulo za kike

Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog

Watoto wa kike wanaotokea kwenye familia duni mara nyingi hukosa kuhudhuria masomo wanapokuwa katika siku za hedhi kutokana na kukosa vifaa salama vya kujihifadhia kama taulo za kile au ‘Pedi’ kama wengi wanavyoita.

Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) inakadiriwa msichana mmoja kati ya 10 kutoka nchi zilizo Kusini mwa Jangwa la Sahara hukosa kwenda shule aingiapo kwenye mzunguko wake wa hedhi.

Kwa wastani wasichana wanaripotiwa kukosa kuhudhuria masomo kuanzia siku 3 hadi tano kwa mwezi yaani kwa mwaka ni siku 36 hadi 60 hali inayochangia kutofanya vizuri katika masomo yao.

Changamoto ya Taulo za kike pia bado inawakabili wanafunzi katika kata ya Mwamala Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga na katika kukabiliana na hali hiyo Halmashauri hiyo imeanza kuchukua hatua kusaidia watoto wa kike.

Afisa Elimu Msingi Halmashauri ya Shinyanga Mkoani Shinyanga Christina Bukoli amesema serikali inalipa kipaumbele suala la taulo za kike ambapo tayari wameliingiza kwenye Bajeti za Halmashauri na wanaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuwapatia wanafunzi taulo za kike.

Bukoli amesema pia kipaumbele kingine ni suala la vyumba vya kujistiri watoto wa kike ambapo maelekezo yaliyopo hivi sasa vyoo vinavyojengwa shuleni ni lazima viwe na chumba cha kujistiri na kwa upande wa suala la taulo za kike.

Afisa Mtendaji wa Kata ya Mwamala, Suzana Kayange ameeleza kuwa kati ya shule tano zilizopo katika kata hiyo (moja ya Sekondari, nne za msingi), chumba cha Usiri kipo katika shule ya msingi Bunonga kilichojengwa na Shirila la Life Water International na shule ya Msingi Igegu kuna chumba cha usiri kilichojengwa na wananchi na kwamba taulo za kike zimekuwa zikitolewa na wadau mbalimbali yakiwemo mashirika.

Nao baadhi ya wanafunzi wameambia Malunde 1 blog kuwa wakati mwingine wanashindwa kuhudhuria masomo yao wanapokuwa kwenye Hedhi hali inayochangia kushuka kwa kiwango cha ufaulu kwenye mitihani kutokana na kukosa mada zinazofundishwa darasani.

"Endapo serikali itatenga bajeti ya taulo za kike, tutahudhuria masomo siku za hedhi na tutasoma kwa kujiamini na hatupata magonjwa ambayo yanaweza kutokea kwa ukosefu wa taulo za kike  lakini pia bajeti hiyo itaziba pengo ambalo wazazi wetu hawawezi kuliziba kwa sababu ya changamoto nyingi zinazowakabili zikiwemo za kiuchumi’’,wameongeza.

Baadhi ya wazazi katika kata ya Mwamala waliozungumza na Malunde 1 blog akiwemo Pius Bundala na Merciana Genea wanashauri kuwe na vyumba vya usiri kwa watoto wa kike na itengwe bajeti ya taulo za kike shuleni badala ya kutegemea misaada ya wadau yakiwemo mashirika.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments