MCHUNGAJI MASEMBO ATAKA UPENDO WA KWELI, KUEPUkA UNAFIKI

Mchungaji Daniel Masembo kutoka Kanisa la EAGT Runzewe akiwasihi waumini kuwa na upendo wa kweli .

Na Mwandishi wetu - Malunde 1 blog

Mchungaji wa Kanisa la Evangelistic Assemblies of God Tanzania (EAGT) Runzewe ambaye pia ni katibu wa kanisa hilo jimbo la Bukombe Mchungaji Daniel Masembo , amewaasa waumini wa kanisa hilo na watanzania kusherehekee siku kuu ya Krismasi (Noeli) kwa kuonyesha upendo kwa watu wote kuliko kuonesha upendo wa kinafiki ambao ni chukizo kwa mwenyezi Mungu.


Mchungaji Masembo amebainisha hayo leo Desemba 25 ,2022 kwenye ibada ya Sikukuu ya Krismasi iliyofanyika katika Kanisa la Evangelistic Assemblies of God Tanzania (EAGT) Ushirika Makimbilio Healing Center mjini Shinyanga.


Amesema Sikukuu ya Krismasi ni sherehe ya kuzaliwa mkombozi Yesu Kristo, hivyo ni vyema watu wakaisherehekea kwa upendo, amani na kusaidia watu wenye uhitaji, na siyo kuonyesha upendo wa kinafiki kwa watu wengine.


“Nawaombeni waumini wa kanisa la Evangelistic Assemblies of God Tanzania (EAGT) Ushirika Makimbilio Healing Center na watanzania wote tusherehekee sikukuu hii ya Krismasi kwa kuonyesha upendo wa kweli kwa watu wote ,na siyo kusherekea sikukuu huku ukiwa na upendo wa kinafiki kwa wenzako ,ukimnafikia mwenzako ipo siku na wewe watakunafikia hadharani,”amesema mchungaji Masembo.


Aidha, amesema Chimbuko la Amani pekee ni kumpokea Yesu Kristo ndani ya mioyo yao na kuonyesha upendo wa kweli , na hakutakuwa tena na migogoro ,mafarakano, na ugomvi katika kanisa na kwenye jamii.


"Kuna watu wako kama Herode wanajifanya wana upendo na wewe kumbe wana upendo wa kinafiki na ndicho chanzo cha mambo yote hayo niliyoyataja ,”ameongeza mchungaji Masembo.


Ibada hiyo imekwenda sambamba na ubatizo ambapo zaidi ya waumini 20 wamebatizwa na kumpokea Yesu Kristo kuwa mwokozi wa maisha yao katika Kanisa la Evangelistic Assemblies of God Tanzania (EAGT) Ushirika Makimbilio Healing Center mjini Shinyanga.
Mchungaji Daniel Masembo akiendelea na Ibada ya Ubatizo.
Mwimbaji Daniel Chaula akisifu na kuabudu.
Mwimbaji Kutoka kwaya ya El Shadai akisifu na kuabudu.

Katibu wa kanisa la EAGT Ushirika Mhandisi Fransis Kuya akimkaribisha mchungaji kwenye ibada.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments