MWAMALA WAJANJARUKA KULAZA WATOTO CHUMBA KIMOJA NA WAGENI.... "HII HAIKUBALIKI SASA, TUNATAKA KUKOMESHA UKATILI"


Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Dorothy Gwajima akizungumza na wananchi wa Mkoa wa Shinyanga na viunga vyake kupitia kipindi maalumu cha Redio Faraja Fm, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia.
Afisa Mtendaji wa kata ya Mwamala Suzana Kayange
Sehemu ya Wakazi wa kata ya Mwamala Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga wakizungumza na Mwandishi wa habari, Kadama Malunde (kulia).

Na Kadama Malunde – Malunde 1 blog
Wakazi wa kata ya Mwamala Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga wameanza kuchukua hatua kudhibiti vitendo vya kuacha kulaza watoto chumba kimoja na wageni ikiwa ni sehemu ya kutokomeza vitendo vya ukatili wa kijinsia dhidi ya watoto.

Wakizungumza na Malunde 1 blog kwa nyakati tofauti wakazi wa Mwamala wamesema hivi sasa wamejanjaruka na kuacha tabia ya kulaza watoto chumba kimoja na wageni ili kudhibiti ukatili dhidi ya watoto.

Mmoja wa wakazi hao Bundala Pius amesema licha ya kwamba ni hatari kulaza watoto chumba kimoja lakini wamekuwa wakilazimika kutokana na uwezo mdogo wa kiuchumi kujenga nyumba kubwa yenye vyumba vingi lakini ili kudhibiti vitendo vya ukatili dhidi ya watoto sasa wameanza kuachana na tabia ya kulaza watoto chumba kimoja na wageni.

“Watoto wasilale chumba kimoja na wageni. Hivi sasa kulaza watoto na wageni hatuwezi kuivumilia, haikubaliki sasa, hatukujua madhara ya kulaza chumba kimoja na wageni”, wamesema Masanja Malale na Ngasa Mhoja.


“Kulaza watoto na wageni siyo vizuri, wageni wengine hawana adabu, hawana maadili, ukiwalaza chumba kimoja na watoto wanawafanyia vitendo vya ukatili ikiwemo kuwabaka na kuwalawiti”,amesema Mboje Malale Luhaga.

Naye Monica James amesema vitendo vya ukatili dhidi ya watoto vimekuwa vikifanywa na ndugu wa karibu hivyo ili kuepuka ukatili dhidi ya watoto ni lazima kudhibiti tabia ya kulaza watoto chumba kimoja na wageni.


Afisa Mtendaji wa kata ya Mwamala Suzana Kayange amesema mwamko huo wa wananchi kuacha kulaza watoto chumba kimoja na wageni unatokana na elimu ambayo serikali kwa kushirikiana na wadau yakiwemo mashirika yamekuwa wakiwapa wananchi katika kutokomeza vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto.

“Tumekuwa tukiwaelimisha wazazi wasilaze chumba kimoja na wageni/ndugu hata kama ni jinsi moja kutokana na kwamba vitendo vya ukatili vimekuwa vikifanywa na watu wa karibu.Tunawaelimisha pia watoto wasilale chumba kimoja na wageni”,amesema Afisa Mtendaji kata ya Mwamala.


Akiwa Mkoani Shinyanga Desemba 5,2022 , Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Dorothy Gwajima alisema ukatili ni ajenda inayohitaji juhudi za pamoja kupinga vitendo hivyo, kwa kuwa takwimu zinaonesha kuwa asilimia 60% ya ukatili wa kijinsia kwa Watoto hutokea majumbani wakati asilimia 40% hufanyika shuleni.


Alisema kuwa Mwaka 2021 Watoto 11,499 walifanyiwa ukatili wa kijinsia ikiwemo kubakwa,kulawitiwa na mimba katika umri mdogo ,hali ambayo inahitaji kuongeza kasi ya kukabiliana na vitendo hivyo ambavyo ni kikwazo dhidi ya maendeleo na ustawi wa jamii.


Dkt. Gwajima alieleza kuwa takwimu za Mwaka 2021 zinaonesha kuwa watoto 5,899 walibakwa, wakati 1,114 walilawitiwa na wengine 1677 walipata mimba katika umri mdogo,vitendo ambavyo watoto wanafanyiwa wakiwa katika mazingira ya nyumbani au shuleni.


“Tunajenga shule ili watoto wasome na kuhitimu lakini wanaishia kupata mimba katika umri mdogo, tafiti zinaonyesha vitendo vya ubakaji na ulawiti hutokea nyumbani kwa asilimia 60,na asilimia 40 hutokea shuleni,serikali haitaweza kujenga shule kwa ajili ya kutunza watoto ili waendelee na kustawi katika maisha yao lakini kumbe huko huko wanabakwa,huko huko wanalawitiwa,lakini ulawiti unaanzia nyumbani walipo Baba,Mama,ndugu na jamaa na baadaye unaenea shuleni kwa watoto wengine ambao pengine wazazi wao wanajitahidi kuwalinda lakini wanakuja kushawishiwa wakiwa katika mazingira ya shuleni”, alisema Dkt. Gwajima.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post