UELIMISHAJI WANANCHI WANAONUFAIKA NA MIRADI YA REA WILAYANI KONDOA


AFISA uhusiano wa Shirika la Umeme Tanzania TANESCO Mkoa wa Dodoma Sarah Libogoma,akitoa elimu ya uhamasishaji kwa wananchi wa vijiji vya Kikilokati, Berabera na Kwahengwa kata ya Kikilo, Kondoa Mkoani Dodoma wanaonufaika na miradi ya umeme wa REA inayoendelea Wilayani Kondoa. 


Mkandarasi kutoka Ok Electrical ndugu Issa Said ,akitoa elimu kwa wananchi kuhusu ushirikishwaji kwenye kazi za uchimbaji za mradi katika maeneo yao. 


Mwananchi wa Barebare akiuliza swali kwa TANESCO juu ya ufafanuzi wa Gharama za mradi wa Umeme 


SEHEMU ya Wananchi wakimsikiliza Afisa uhusiano wa Shirika la Umeme Tanzania TANESCO Mkoa wa Dodoma Sarah Libogoma,wakati akitoa elimu ya uhamasishaji kwa wananchi wa vijiji vya Kikilokati, Berabera na Kwahengwa kata ya Kikilo, Kondoa Mkoani Dodoma wanaonufaika na miradi ya umeme wa REA inayoendelea Wilayani Kondoa. 

........................................... 

Na.Mwandishi Wetu-KONDOA 

SHIRIKA la Umeme Tanzania TANESCO Mkoa wa Dodoma limeendelea na zoezi la uelimishaji na uhamasishaji katika vijiji vinavyonufaika na miradi ya umeme REA inayoendelea Wilayani Kondoa kupitia wakala wa Nishati vijijini REA. 

Elimu hiyo kwa umma imehusisha kufahamisha wananchi juu ya miradi ya REA na utekelezaji wake, uepukaji vishoka pamoja na matumizi sahihi ya umeme wenyewe ikiwemo uzingatiaji wa usalama kwanza. 

Akiongea katika vijiji vya Kikilokati, Berabera na Kwahengwa kata ya Kikilo, Kondoa Mkoani Dodoma, Afisa uhusiano wa TANESCO Mkoa wa Dodoma,Sarah Libogoma amewataka wananchi kupokea mradi unaoendelea kwenye maeneo yao kwa kuhakikisha wote waliofikiwa na awamu hii wanajitokeza kuomba huduma kupitia Mfumo wa NiKONEKT kwa ufanisi Zaidi kupitia simu zao kadri Serikali ilivyokusudia kwani gharama za mradi huo zimepunguzwa sana kwa Mwananchi. 

"Kwa shilingi 27,000 unakuwa umepata huduma kwa pesa ambayo ukiuza kuku wawili unaunganisha huduma ya umeme milele kwenye nyumba yako hivyo ni vyema kuhakikisha tunatumia fursa hii vizuri kwani umeshawashwa na mradi upo ukingoni kukamilika." Alisema Libogoma Pia wananchi wamehimizwa kuepuka udanganyifu unaoweza kujitokeza kipindi chote cha mradi na kutoa taarifa mara moja kwa mamlaka za serikali zilizopo katika maeneo yao. 

Aidha, wananchi wametakwa kuzingatia usalama katika matumizi ya umeme ikiwamo, kutofanya shughuli zozote chini au karibu na miundombinu ya umeme kama vile Transfoma, kuhakikisha wanatumia mafundi wanaotambulika katika 'Wiring' ya nyumba zao pamoja na kutokata miti iliyo karibu na nyaya za umeme bila kushirikiana uongozi ili kuepusha madhara yanayoweza kujitokeza. Hata hivyo Libogoma kupitia uhamasishaji huo katika vijiji vyote ameendelea kusisitiza utunzaji wa miundombinu ya umeme kwani serikali inatumia gharama nyingi katika kupeleka miradi katika maeneo hayo kwa manufaa ya wananchi wake wote hivyo ulinzi wa mali hizi ni shirikishi. 

Kwa upande wake Diwani wa kata ya Kikilo Ndugu Yuda Daniel ameishukuru Serikali kwa kupeleka miradi hiyo kwakuwa kilikuwa kilio kikubwa kwa wananchi wapate umeme huku akisisitiza wananchi kutoa ushirikiano kwa wakandarasi ili kufanikisha miradi hiyo. 

“Wananchi wana matumaini makubwa na Serikali yao hivyo naamini watatoa ushirikiano wa kutosha kwani wamefurahia mno kufikiwa na mradi huu,” 

Nao wananchi wa vijijini hivyo akiwemo Hamisi Said wa Kijiji cha Kwahengwa na Karimu Msondo wa keikei wameishukuru TANESCO kwa kufika na elimu hii, pia shukrani zimetolewa kwa Serikali kwa kusogeza huduma na kuomba kuendelea kufikiwa kwa vile vitongoji ambavyo bado navyo Serikali ivikumbuke. 

Uhamaishaji huu umefanywa na TANESCO kwa kushirikiana na Mkandarasi Ok Electrical anayetekeleza mradi huo kwenye vijiji 72 vya wilaya za Kondoa na Mpwapwa ambaye hadi sasa ameshatekeleza takribani asilimia 50 ya mradi huo. Mradi huu unatarajia kumalizika January 2023, ambapo katika Wilaya ya Kondoa pekee Vijiji 14 kati ya vijiji 34 vimewashwa, huku Kazi ya kuwasha ikiendelea katika vijiji 20 vilivyobakia.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments