CHADEMA WAPINGA TUME YA MKUU WA MKOA WA SHINYANGA UCHUNGUZI BWAWA LA MGODI WA MWADUI KUPASUKA, TOPE KUZAGAA KWA WANANCHI


Muonekano wa Tope likiendelea kusambaa kwenye makazi ya watu, mara baada ya bwawa la Mgodi wa Almasi Mwadui Kupasuka leo asubuhi, na kusababisha athari kwa wananchi

 CHAMA CHA DEMOKRASIA NA MAENDELEO (CHADEMA) MKOA WA SHINYANGA.

TAARIFA KWA UMMA


*Tamko la kupinga uundwaji wa Tume ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Kuchunguza kupasuka na athari za kimazingira kwa Bwawa la Maji machafu la Mgodi wa Almasi wa Mwadui.*


Mnamo tarehe 07.11.2022 Bwawa la kuhifadhia maji machafu la mgodi wa Mwadui lilipasuka na kusababisha maji na matope kuzagaa kwenye vijiji vya Ng’wang'holo na Nyenze, Kata ya Mwadui Lohumbo Wilaya ya Kishapu, Shinyanga.


Aidha, Maji machafu na tope yamesambaa katika eneo la zaidi ya kilometa nane na kuathiri sana nyumba kadhaa, mashamba, mifugo, mimea, visima na hata baadhi ya watu kuathirika kiafya.


Mara baada ya kutokea kwa hali hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mh Sophia Mjema amejitokeza kwenye vyombo vya habari akisema ameunda Tume ya watu kutoka kamati yake ya ulinzi na usalama, baadhi ya wataalamu na kushirikiana na wataalamu wa mgodi wa Mwadui. Na kwamba wanajukumu la kutazama chanzo cha kupasuka kwa Bwawa hili, kufanya tathmini za athari na mwisho kuangalia namna jambo hili lisijirudie.


CHADEMA Mkoa wa Shinyanga tunapinga uundwaji wa Tume hiyo na Mkuu wa Mkoa, kwa kuzingatia aina ya wajumbe pamoja na hadidu za rejea kwa Tume Kwa sababu;


Mosi, kwa mujibu wa muundo wa serikali, Nchi yetu tuna wizara ya Muungano na Mazingira ambayo ina majukumu ya kutazama mazingira na ipo chini ya Ofisi ya Makamu wa Rais na Waziri wake ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira hivyo ni busara wizara hii ikahusika na jambo hili nyeti ambalo mpaka sasa limeathiri makazi na mali nyingi za wananchi.


Kwamba, tuna Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) ambalo limeanzishwa kwa mujibu wa Sheria ya Taifa ya usimamizi wa Mazingira namba 19 ya Mwaka 1983. Kwamba Baraza hili lina jukumu la usimamizi wa mazingira.


Kwamba, Kifungu cha 17 cha Sheria hiyo, inaipa NEMC majukumu pamoja na Kutekeleza shughuli za uzingatiaji na usimamizi (enforcement and compliance) wa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira; 

NEMC inawajibu wa Kusimamia mchakato wa Tathmini ya Athari kwa Mazingira (TAM) na kushirikisha umma na si ofisi ya Mkuu wa Mkoa.


Aidha, Kifungu cha 18(2) cha Sheria ya Usimamizi wa mazingira inatoa mchanganuo mpana wa majukumu ya NEMC ambayo kwayo tunaamini wanaweza kuja na majibu sahihi juu ya nini kimetokea.


CHADEMA, tunajiuliza kama NEMC ilitekeleza wajibu wake kwa kufanya uhakiki wa mazingira wa mara kwa mara kwenye Bwawa hilo yaani Environmental Audit. Lakini pia kama kulikuwa na ukaguzi na ufuatiliaji yaani Audit and Monitoring katika Bwawa hilo na Mgodi wote kwa ujumla.


Kwani tunaamini lengo la kuanzishwa kwa NEMC ni kulinda na kuthibiti ajali kama hizi zinazoweza kusababisha uharibifu mkubwa wa kimazingira kama huu kwani kwa taarifa za awali tumeelezwa ni zaidi ya Nyumba13, zimezingirwa na tope na zingine kudondoka, huku ikisadikiwa watu zaidi ya 50 kuathirika kwa kukosa malazi na chakula mpaka sasa, na watoto wapatao wanne wakiwa wanaumwa.


CHADEMA tunasikitika kwa kutokuchukuliwa hatua mahsusi na za haraka kwa wahanga hawa, ambao hawana makazi na chakula huku wakiwa wamepoteza mifugo na hawana hata sehemu ya kupata maji ya kunywa. Tunaitaka Serikali na Mgodi wa Mwadui kuwatafutia sehemu salama za kuishi kwa muda na kuwapatia waathirika wote hudumu muhimu za kibinadamu.


Mwisho tunatoa wito kwa Serikali, kuivunja tume hii na jukumu hili lifanywe na Wizara ya Muungano na Mazingira kwa kushirikiana na NEMC pamoja na wadau na wataalamu wa mazingira nchini, kwani tunaamini tope na maji hayo yatakuwa na athari kubwa kwa jamii yetu. CHADEMA tunaendelea kufuatilia kwa ukaribu jambo hili, na kuona hatua kali zikichukuliwa, pamoja na kuangazia stahiki zote za waathirika.


Imetolewa leo Alhamisi 10 Novemba, 2022 na

Emmanuel Ntobi, 

Mwenyekiti wa CHADEMA Mkoa wa Shinyanga.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post