Kile ambacho kilipaswa kuwa ibada nzuri ya Jumapili mbele za Mungu kiligeuzwa kuwa fujo na uharibifu wa mali ya kanisa yenye thamani ya mamilioni ya shilingi.
Kundi la washambuliaji likiongozwa na Kamishna wa Polisi Henry Njoku aliyekuwa na bunduki pia walimfanyia vurugu kasisi Emmanuel Samuel Bares, mwangalizi mkuu wa Kanisa la Higherlife nchini Nigeria.
Katika mahojiano na Legit TV, Emmanuel alifichua kuwa tukio hilo lilianza saa moja asubuhi wakati akielekea kanisani na familia yake huku akipigiwa simu kuwa kulikuwa na tingatinga kwenye kiwanja hicho.
“Niliwauliza hao watu ni akina nani wakasema hawajui, nikawaambia wachukue video na wanitumie picha hizo tukiwa bado tunakuja, wakasema simu zao zilikuwa zimechukuliwa hivyo basi hakuna jinsi wangerekodi matukio," alisema.
Kupitia mazungumzo ya simu, mtumishi huyo wa Mungu alionyesha kwamba lengo la kuvamiwa lilikuwa ni kuangusha hekalu wakati walianza kubomoa jengo hilo kabla hajafika.
Mchungaji alipofika kanisani, yeye pia alivamiwa na vijana hao waliokuwa na hamaki.
“Niliingia ndani ya kanisa kusali na kumshukuru Mungu, wakanishikilia pale, wakanichana nguo zangu na kuanza kunipiga, wakaniburuza chini jinsi ilivyonekana kwenye video,” aliendelea na kuongeza kuwa alipokea kichapo kikali ndani ya kanisa.
Mchungaji alionyesha kusikitishwa na ukweli kwamba kanisa halikupewa karatasi zozote za korti au notisi ya kuondoka, walionekana tu kuvamiwa na hekalu kubomolewa.
Kasisi huyo alidokeza kuwa hema lililoharibiwa pekee lilikuwa la thamani ya mamilioni, bila kusahau vifaa vilivyomgharimu zaidi ya N15 milioni (KSh 4.1m), pamoja na ala za muziki na viti.