TCRA YATAJA MIKOA MITANO INAYOONGOZA MATUMIZI YA LAINI ZA SIMU...WATUMIAJI WA INTANETI WAONGEZEKA


Mkurugenzi Mkuu wa TCRA Dkt.
Jabiri Kuwe Bakari akizungumza na Waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusu ripoti ya utendaji wa Sekta hiyo Kwa robo mwaka.

Na Dotto Kwilasa,Malunde 1 blog DAR ES SALAAM

MAMLAKA ya mawasiliano Tanzania (TCRA)imesema inaendelea kuweka mazingira wezeshi ili kuhakikisha watoa huduma wanaendelea kutoa huduma kwa ufanisi,weledi na ubora hali itakayo 
saidia kukidhi mahitaji ya jamii kwa maendeleo ya uchumi kidigitali.

Hayo yameelezwa leo Jijini Dar Es Salaam na Mkurugenzi Mkuu wa TCRA Dkt.Jabiri Kuwe Bakari wakati akizungumza na Waandishi wa habari kuhusu ripoti ya  utendaji wa Sekta hiyo wa kila robo mwaka na kueleza kuwa ripoti hiyo ya utendaji inaonesha ongezeko la asilimia 3.4 kwa laini za simu zinazotumika.

Amefafanua kuwa hadi mwezi Juni 2022 kulikuwa na laini milioni 56.2 idadi iliyoongezeka hadi kufikia laini milioni 58.1 Septemba 2022 na kwamba idadi hiyo inahusisha laini zinazotumiwa na watu na laini zinazotumiwa kwa ajili ya mawasiliano katika mashine na mashine(M2M).

Amesema takwimu zinaonesha mikoa mitano Tanzania inayoongoza kuwa na idadi kubwa ya laini za simu zinazotumika hadi Septemba 2022 ni Dar Es Salaam(Laini milioni 9,756,697),Mwanza (Laini 3,700,914),Arusha(laini 3,448,200),Mbeya(laini 3,089,848)na Tabora(laini 3,060,407).

"Uchambuzi wa laini hizo kwa watoa huduma unaonesha kuna ushindani mkubwa kwani hakuna mtoa huduma mwenye zaidi ya asilimia 35 ya laini zilizosajiliwa,"amesema

Mkurugenzi huyo wa TCRA pia ameeleza kuwa mwelekeo wa usajili kwa miaka mitano iliyopita unaonesha ongezeko la asilimia nane kwa mwaka na kufafanua kuwa kuenea kwa laini miongoni mwa watu kumeongezeka kwa asilimia nne kwa mwaka.

"Kuenea kulikuwa ni asilimia 78 mwaka 2017, asilimia 81 mwaka 2018 , asilimia 88 mwaka 2020 na asilimia 91 mwaka 2021,"amesema.

Kuhusu gharama za vifurushi vya data na simu , Mkurugenzi huyo amesema wastani wa gharama za vifurushi vya simu zilikuwa Shilingi 7.8 Kwa kupiga ndani ya mtandao mwezi Septemba 2022,kutoka Shilingi 7.7 juni 2022.

Pamoja na ongezeko hilo amesema gharama bado ni chini kulinganisha na vifurushi vya simu kwenda mitandao mingine ambapo wastani wa vifurushi vya simu kwenda mitandao mingine ulikuwa Shilingi 8.1 Septemba 2022 ikiwa ni ongezeko kutoka Shilingi 7.6 juni 2022.

"Pamoja na hayo wastani wa gharama za data September 2022 zimebaki kuwa Shilingi 1.8kwa MB kama ilivyokuwa Juni 2022,"amesema

Wakati huo huo amezungumzia idadi ya watumiaji wa intaneti kuwa imeongezeka kutoka 29,169,958 Juni 2022 hadi 31,122,163 Septemba 2022 sawa na ongezeko la asilimia 6.7.

"Mwelekeo wa ongezeko la watumiaji wa intaneti linaonesha kulikuwa na ukuaji wa Takribani asilimia 17 Kila mwaka Katika kipindi cha miaka mitano ambapo mwaka 2017 kulikuwa na watumiaji zaidi ya milioni 16 na mwishoni mwa mwaka 2021 kuliongezeka kufikia zaidi ya milioni 29,"amefafanua Dkt.Bakari.

Vilevile ameeleza kuwa matumizi ya intaneti yameongezeka kutoka wastani wa MB 6,037 Kwa watumiaji Machi 2022 hadi  MB 6,626 Kwa watumiaji Septemba 2022.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post