TBS YAWAFUNDA WAJASIRIAMALI BABATI


Na Mwandishi Wetu, Manyara

WAJASIRIAMALI nchini wameendelea kuelimishwa kuhusiana na umuhimu wa kuthibitisha ubora wa bidhaa zao hatua ambayo itawasaidia kupata masoko ya uhakika na hivyo kuondokana na vikwazo vya kibiashara ambavyo wamekuwa wakikabiliana navyo.

Akizungumza na wajasiriamali wakati wa Maonesho ya Biashara ya Tanzanite yaliyofanyika katika Uwanja wa Kwaraa, Babati Mjini mkoani Manyara, mwishoni mwa wiki, Kaimu Mkuu wa Kanda ya Kaskazini wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS) Deogratius Ngatunga, alisema wameshiriki Maonesho hayo kwa ajili ya kutoa elimu kwa wajasiriamali, wadau na wananchi kwa ujumla kuhusiana na umuhimu viwango.

Alisema maonesho hayo ambayo yameandaliwa na Chama cha Biashara, Viwanda na Kilimo (TCCIA) yamekuwa fursa nzuri kwa shirika, kwani limetoa elimu kwa wajasiriamali kuhusiana na umuhimu wa kuthibitisha ubora wa bidhaa wanazozalisha.

Alifafanua kwamba shirika hilo limekuwa likithibitisha ubora wa bidhaa zinazozalishwa na wajasiriamali bure, hivyo aliwataka kujitokeza kwa wingi kuchangamkia fursa hiyo.

Ngatunga alifafanua kwamba wajasiriamali wanatakiwa kupitia SIDO kwa ajili ya kupata barua ya utambulisho na wakiishaifikisha TBS, mchakato wa kuthibitisha ubora wa bidhaa unaanza mara moja.

Kuhusu faida za kuthibitisha ubora wa bidhaa, Ngatunga alisema inawaondolea vikwazo vya kibiashara vinavyotokana na bidhaa zao kutokubalika kwenye masoko.

Alisema bidhaa iliyothibitisha na TBS inamhakikishia mlaji usalama wa afya yake, ndiyo maana watu wengi wakitaka kununua bidhaa kwanza wanataka kujiridhisha kama ina alama ya ubora ya shirika hilo.

"Hii ina maana kwamba kama bidhaa yako hajathibitisha haitapata wanunuzi, watu wanakuwa na mashaka nayo. Sasa ili watu wasiwe na mashaka tumewahimiza waje TBS kuthibitisha bidhaa zao bure," alifafanua Ngatunga.

Aidha, alisema nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki zina makubaliano ambapo bidhaa ikishathibitisha na shirika la viwango la nchi ilikozalishwa haitakiwi kuthibitishwa tena inapotoka nje ya mipaka ya nchi hiyo.

"Kwa hiyo, hiyo ni fursa nzuri kwa wazalishaji kupata uhakika wa masoko, kwani alama ya ubora inaondoa vikwazo vya kibiashara," alisema.

Kwa upande wa wananchi waliohudhuria maonesho hayo, walihimizwa kununua bidhaa ambazo zimethibitishwa na TBS. Aidha walitakiwa kuhakikisha wanaangalia muda wa mwisho wa matumizi wa bidhaa wanazotaka kuzinunua.

Kupitia maonesho hayo mbali na kutoa elimu maofisa wa TBS walitatua changamoto mbalimbali ambazo wananchi walieleza kukabiliana nazo.

Kufuatia elimu iliyotolewa kwenye maonesho hayo, wajasiriamali wengi waliahidi kuanza mchakato wa kuthibitisha bidhaa zao na kuwa mabalozi kwa wengine ambao hawakupata fursa hiyo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post