MWL. NYERERE KUNG'ARA FILAMU ZA KIMKAKATI


Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania Dkt.Kiagho Kilonzo.

Na Dotto Kwilasa ,DODOMA.

SERIKALI kupitia Bodi ya filamu nchini ina mpangowa kuanzisha  filamu za Kimkakati zitakazo saidia kutunza kumbukumbu za kihistoria kwa kuhusisha taarifa za viongozi  mbalimbali hatua itakayo saidia kwa kiasi kikubwa kujenga mapenzi hasa kwa vijana wa kitanzania kwa nchi yao kwa kuwaongezea ufahamu wa rasilimali waliyonayo. 


Hayo yameelezwa leo Jijini hapa na Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania Dkt.Kiagho Kilonzo wakati akilezea utekelezaji wa shughuli mbalimbali za Bodi hiyo pamoja na mwelekeo wa utekelezaji kwa mwaka wa fedha 2022/2023 huku akimtaja Mwl. Julius Kambarage Nyerere kuwa alisaidia ukombozi wa nchi mbalimbali barani Afrika hivyo atakuwa wa kwanza kupewa kipaumbele Katika filamu hiyo.


Amesema program hiyo ina lengo la kuratibu uandaaji wa filamu zenye maudhui ya kutangaza utajiri wa nchi katika eneo la utamaduni, historia na jiografia.


"Tumeshuhudia Viongozi mbalimbali mashuhuli tayari wameenziwa kupitia filamu mfano Idd Amin, Nelson Mandela na wengine lakini kwetu sisi Bado hatujamuenzi Mwalimu Nyerere nadhani Sasa huu ni wakati wake,"amesema


Pamoja na hayo amesema Bodi hiyo ya filamu pia itaanza kurudisha utamaduni wa kutazama filamu katika Kumbi za Sinema itakayorudisha hadhi ya michezo ya kuigiza hatua  inatarajiwa pia kutoa mchango stahiki katika uchumi wa wadau wa Sekta na Taifa kupitia viingilio vya mlangoni. 


Akizungumzia fursa za Ajira ya filamu nchini amesema kwa kipindi cha Januari hadi Disemba, 2021 pekee inakadiriwa kuwa ilichangia takriban ajira 30,000 zilizotokana na Filamu (waigizaji, waandaaji na watoa huduma) ambapo kwa mazingira ya Kitanzania, Filamu moja (wastani wa watu 20, tamthilya moja wastani wa watu 100) kiasi ambacho ni ongezeko la nafasi 5,000 kutoka 25,000 kiasi kinachokadiriwa kuzalishwa mwaka 2020. 

 

"Katika uratibu wa matukio ya Tasnia mwaka 2021 Serikali ilifanya TAMASHA LA TUZO ZA FILAMU ambalo kilele chake kilifanyika jijini Mbeya Tarehe 18 Disemba, 2021 na kutunuku Tuzo na zawadi kwa watu 30 waliofanya vizuri zaidi katika vipengele mbalimbali kwenye eneo la Filamu ambapo mwaka huu Tamasha hilo linatarajia kuzinduliwa na Waziri mwenye dhamana mwezi huu wa Oktoba na kufikia kilele chake mwezi Disemba, 2022,"amesema. 


Ameema katika kufikia malengo Serikali imewezesha Shirikisho hilo kuongeza weledi na ubora wa filamu Kwa kuweka mazingira rafiki ya uwekezaji,kuimarisha mahusiano ya kikanda na kimataifa,kuongeza ushindani kwenye kazi za filamu,kurasimisha biashara na shughuli za filamu na kulinda haki za wasanii.


Akizungumzia kuhusu kusimamia haki na Maslahi ya Wasanii ameeleza kuwa Bodi ya Filamu inaratibu Kamati Maalum ya kutetea Haki za Wasanii iliyoundwa na Waziri mwenye dhamana ya kusimamia maswala ya Sanaa nchini kwa mara ya kwanza mwaka 2018 na kuhuishwa tena 2019 na 2020 (ikiwa na mabadiliko ya baadhi ya wajumbe) itakayodumu hadi mwishoni mwa mwaka 2022. 


"Hadi sasa Kamati imeshapokea malalamiko 30 na kuyashughulikia, ambapo takriban shilingi milioni 300 zilizokuwa zimedhulumiwa zimesharejeshwa kwa wasanii,Malalamiko 22 yamesuluhishwa, na Malalamiko 8 yapo katika hatua mbalimbali za kushughulikiwa hata hivyo baadhi ya malalamiko yaliyopokelewa na kushughulikiwa ni yale ya marehemu Amri Athumani (King Majuto), marehemu Steven Kanumba, msani David Ganzi (Young Dee), Mzalishaji wa Tamthilya Samwel Isike,"amesema 


Katika kuwajengea uwezo wanatasnia ya filamu nchini amesema Taasisi imekuwa ikiandaa programu mbalimbali za mafunzo ya vitendo, darasani na yale ya mdahalo katika maeneo mbalimbali ya nchi ikiwemo mafunzo ya vitendo ambapo Mwaka 2021 na 2022 Taasisi iliandaa mafunzo hayo kwa mikoa ya Dar (75), Geita (30) na Dodoma (30), na kunufaisha watu 135, walioishia kuandaa filamu fupi fupi wakiwa mafunzoni. 


Pamoja na mambo mengine amebainisha kuwa Bodi hiyo inaendelea na majukumu yake kwa kuishauri Serikali masuala yote yanayohusu Filamu na Michezo ya Kuigiza pamoja na kuratibu Sekta ya Filamu na Michezo ya kuigiza na usimamia na kuratibu utayarishaji/uandaaji, uhakiki wa Filamu na Michezo ya Kuigiza pamoja na kuzipangia madaraja na kuzipa vibali.


Amesema katika utekelezaji wa shughuli za Bodi hiyo mfumo wa kutoa huduma kidigitali  kwa wadau wake (bila kulazimika kufika katika ofisi za Bodi) ikiwemo vibali mbalimbali (uandaaji wa filamu, uhakiki, vitambulisho, kuhifadhi taarifa za wadau na kuwatambua kupitia vitambulisho vinavyotolewa na Bodi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post