KAZI YA UCHUKUAJI DATA KITALU CHA RUVUMA YAKAMILIKA


Meneja wa mradi wa uchukuaji wa data za mitetemo za 3D katika Kitalu cha Ruvuma, Bw. Stan Schlesinger akitoa maelezo mafupi ya maendeleo ya mradi huo mara baada ya Bodi ya Wakurugenzi ya PURA kutembelea eneo hilo tarehe 09 Oktoba 2022.

Meneja Uzalishaji wa Gesi Asilia kutoka TPDC, Mha. Felix Nanguka akitoa historia fupi kwa Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa PURA kuhusu ugunduzi wa gesi asilia katika Kitalu cha Ruvuma. Mha. Felix pia alieleza mikakati iliyopo ya kuendeleza gesi hiyo ili kufikia lengo la kuanza uzalishaji mwaka 2024/25.

****************************

Kampuni ya ARA Petroleum Tanzania Ltd imeeleza kuwa kazi ya uchukuaji wa data za mitetemo za 3D katika Kitalu cha Ruvuma kilichopo Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara imekamilika kwa asilimia 100.

Kampuni hiyo ambayo ni mwendeshaji wa Kitalu hicho imeeleza hayo leo wakati Bodi ya Wakurugenzi ya PURA ilipotembelea eneo hilo kwa lengo la kuongeza uelewa wa shughuli zinatokekelezwa na kampuni hiyo.

Akizungumza kwa niaba ya Kampuni ya ARA, Meneja wa mradi huo wa uchukuaji wa data, Bw. Stan Schlesinger alisema kuwa kazi ya uchukuaji wa data za mitetemo ilianza rasmi mwishoni mwa mwezi Julai, 2022 na kwamba kazi hiyo ilitanguliwa na kazi za awali ikiwemo usafishaji wa njia zilizotumika wakati wa uchukuaji wa data. Kazi za awali zilianza Januari, 2022.

“Kwa sasa kunachoendelea ni kuvuna data kutoka katika vifaa vilivyotumika wakati wa ukuchuaji wa data (nodes) na kurejesha mazingira katika hali yake ya awali (restoration). Data zilizokusanywa zitachakatwa na kutafsiriwa kabla ya kuendelea na hatua ya uchimbaji wa visima, kazi ambayo itafanyika mwakani” aliongeza Bw. Stan.

Mbali na maelezo hayo, Bw. Stan aliijulisha Bodi kuwa mradi wa uchukuaji wa data za mitetemo katika Kitalu cha Ruvuma umekuwa na manufaa kadha wa kadha kama vile ajira kwa watanzania takribani watanzania 160. Aidha, kupitia mradi huo watanzania walipata pia fursa za kutoa huduma mbalimbali zilizohitajika wakati wa mradi kama vile usafiri, malazi, ulinzi, chakula, uthaminishaji, mafuta na mitambo n.k

Akizungumza kwa niaba ya Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya PURA, Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Bw. Halfani R. Halfani aliipongeza ARA Petroleum kwa kazi kubwa na nzuri iliyofanyika. Aidha, Bw. Halfani alieleza kuwa matumaini ya Bodi, PURA na Serikali kwa Ujumla ni kuona gesi asilia iliyogunduliwa katika Kitalu cha Ruvuma inaendelezwa mapema ili kupata gesi asilia kwa matumizi mbalimbali nchini.

Ugunduzi wa gesi asilia katika Kitalu cha Ruvuma ulifanyika mwaka 2012 ambapo kiasi cha futi za ujazo trilioni 0.466 kiligunduliwa. Mipango ya uendelezaji wa gesi hiyo ipo katika hatua mbalimbali na matumaini ni kuanza uzalishaji ifikapo mwaka 2024/25.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post