WALIMU WALIA NA UHABA WA NYUMBA BAGAMOYO


Katibu wa CWT Wilaya ya Bagamoyo akikabidhi risala ya chama kwa mgeni rasmi ,Katibu Tawala Wilaya ya Bagamoyo Bi. Kasilda Mgeni


NA. ELISANTE KINDULU, BAGAMOYO

NYUMBA za walimu zimetajwa kuwa miongoni mwa kero zinazoihusu sekta ya Elimu katika Wilaya ya Bagamoyo ,mkoa wa Pwani imefahamika.

Hayo yamebainishwa na Mwenyekiti wa chama Cha walimu Tanzania(CWT) Wilaya ya Bagamoyo Mwalimu Hamisi Kimeza ,alipokuwa akimkaribisha Katibu Tawala wa Wilaya ya Bagamoyo Bi. Kasilida Mgeni katika mkutano mkuu wa chama hicho Wilaya ya Bagamoyo uliofanyika katika ukumbi wa shule ya Sekondari Bagamoyo.

Mwalimu Kimeza ameiambia hadhira ya mkutano huo kuwa licha ya Serikali kufanya vizuri kwenye malipo ya nauli za likizo kwa walimu lakini bado inahitaji kufanya juhudi hizo hizo katika changamoto zingine zinazomkabiri Mwalimu ikiwemo uhaba wa nyumba za walimu.

Akizitaja kero zingine katika risala ya chama hicho, Katibu wa CWT wa Wilaya hiyo Mwalimu Shaaban Tesua amesema walimu wamekuwa wakisubiri malipo ya fedha za mapunjo ya mshahara baada ya kupanda madaraja yao kwa Muda mrefu Sasa, fedha za uhamisho na baadhi ya walimu wa halmashauri ya Chalinze kusomeka Bagamoyo na wa Bagamoyo kusomeka Chalinze.

Akimwakilisha mkuu wa wilaya ya Bagamoyo ambaye alikuwa Mgeni rasmi Katibu Tawala wa Wilaya hiyo Bi. Kasilda Mgeni, alisema amezichukua changamoto zote za walimu na kuwahakikishia atazifikisha mahali sahihi kwa utekelezaji.

Aidha Katibu Tawala huyo alitumia fursa hiyo kumpongeza Katibu wa CWT Wilaya ya Bagamoyo kwa juhudi zake za kufika katika ofisi yake kufuatilia haki mbalimbali za walimu katika Wilaya yake. 

Mkutano huo mkuu ulishirikisha wawakilishi wa CWT mahala pa kazi kutoka katika halmashauri ya Chalinze na Bagamoyo mkoa wa Pwani.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post