YALIYOJIRI KATIKA TAMASHA LA JINSIA KANDA YA KASKAZINI 2022

 

Rose Mwalongo Ngunangwa akiwasilisha taarifa ya mambo yaliyojiri kwa niaba ya TGNP wakati wa Tamasha la Jinsia Kanda ya Kaskazini Ijumaa Oktoba 7,2022 lililofanyika kwa muda wa siku tatu (Oktoba 5-7,2022) katika viwanja vya Kwasa Kwasa Wilaya ya Same Mkoani Kilimanjaro.

Mkuu wa wilaya ya Same Mkoani Kilimanjaro Mhe. Edward Mpogolo akizungumza wakati akifunga Tamasha la Jinsia Kanda ya Kaskazini  Ijumaa Oktoba 7,2022 lililofanyika kwa muda wa siku tatu (Oktoba 5-7,2022) katika viwanja vya Kwasa Kwasa Wilaya ya Same Mkoani Kilimanjaro.
Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP, Lilian Liundi  akizungumza wakati wa kufunga Tamasha la Jinsia Kanda ya Kaskazini Ijumaa Oktoba 7,2022 lililofanyika kwa muda wa siku tatu (Oktoba 5-7,2022) katika viwanja vya Kwasa Kwasa Wilaya ya Same Mkoani Kilimanjaro.
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Mhe. Nurdin Babu akifurahia jambo na washiriki wa Tamasha la Jinsia Kanda ya Kaskazini.TAARIFA KWA UMMA

Yaliyojiri katika Tamasha la Jinsia Kanda ya Kaskazini

Tarehe 5-7 Oktoba 2022, Wilaya ya Same, Kilimanjaro 

“Haki ya Uchumi: Rasilimali Ziwanufaishe Wananchi Walioko Pembezoni”

 

Kuanzia tarehe 5 Oktoba hadi 7 Oktoba 2022 Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) kwa kushirikiana na mashirika mbalimbali yanayotetea haki za wanawake na usawa wa jinsia, wanaharakati binafsi na kwa ufadhili wa Ubalozi wa Watu wa Kanada, na Uswidi, umefanya Tamasha la Jinsia la Kanda katika Viwanja vya Kwasa Kwasa hapa Wilayani Same, Mkoani Kilimanjaro.


Tamasha la Jinsia la Kanda limeongozwa na mada kuu isemayo,Haki ya Uchumi: Rasilimali Ziwanufaishe Wananchi Walioko Pembezoni’, huku mada ndogo ndogo zikiangazia fursa za kilimo, uongozi shirikishi, mila kandamizi, huduma za kijamii (afya ya uzazi), na ujenzi wa nguzu za pamoja yaani TAPO.


Tamasha la Jinsia la Kanda limekutanisha zaidi ya washiriki 500 wanaojumuisha wadau wa maendeleo (Ubalozi za Uswidi, Ubalozi wa Canada, Global Affairs Canada, Chuo cha Coady, SeedChange, Crossroads International, Aga Khan Foundation, ONGAWA), sekta binafsi, asasi za kiraia, vikundi vya kijamii na wanaharakati ambao wamekuwa bega kwa bega na TGNP katika kuchagiza usawa wa jinsia. Serikali ya Jamhuri ya Tanzania imeshiriki kupitia TAMISEMI na Wizara ya Maendeleo ya Jamii.


Mkurugenzi wa TGNP, Bi. Lilian Liundi kwa niaba ya Bodi ya Wakurugenzi na Wanachama alitoa usuli kuhusu Tamasha la Jinsia la Kanda ikiwa ni muendelezo wa mkakati wa taasisi tokea mwaka 1996 kuunganisha sauti ya pamoja na kutekeleza mikakati ya kufikia usawa wa kijinsia. TGNP imefanya matamasha 14 kitaifa na katika ngazi ya wilaya kwa mafanikio makubwa ya kufikia washiriki 31,000 (70% wanawake na 30% wanaume) na kushawishi mabadiliko. Hivyo, Tamasha limekuwa sehemu ya kuendelea kutanua harakati za ujenzi wa nguvu za pamoja nchini na kutoa fursa kwa watu wengi zaidi kushiriki.


Mgeni Rasmi wa Tamasha la Jinsia la Kanda, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Mheshimiwa Nurdin Babu katika neno la ufunguzi alitambua mchango wa TGNP katika kuwainua wanawake kiuchumi na kuongeza ushiriki wao kwenye nafasi za uongozi na ngazi za maamuzi.


Aidha, akipinga ukatili wa kijinsia mkoani Kilimanjaro, Mheshimiwa Nurdin Babu aliweka wazi nia ya dhati kukomesha vitendo vya ukatili kwa kuelekeza wananchi kufika ofisini kwake bila kusita. Aidha, alitoa maelekezo kwa Mkuu wa Wilaya ya Same kuwasilisha Agenda ya Masoko kwa Wanawake Wakulima wa Tangawizi kwenye Mkutano wa Baraza la Biashara la Mkoa lililopangwa kufanyika tarehe 6 Oktoba 2022. 


Pia kuunga mkono jitihada za wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, ameelekeza Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmshauri ya Wilaya ya Same kuendeleza utoaji wa mikopo, kuondoa urasimu, na kuongeza kiwango cha mikopo hiyo ili kuwakwamua kiuchumi.


Katika siku ya pili ya Tamasha, washiriki walijikita kwenye tafakuri na mijadala kupitia warsha zilizoangazia maeneo muhimu manne (4): Haki ya Uchumi; Huduma za Kijamii (Afya ya Uzazi); Uongozi Shirikishi; na Mila Kandamizi. 


Kwa ujumla, changamoto zilizotambuliwa katika maeneo hayo ni pamoja na upatikanaji na urasimu kufikia mikopo na mitaji ya biashara kwa wanawake, ukosefu wa masoko na bei za uhakika kwa mazao kama tangawizi, uhaba wa taarifa juu ya afya ya uzazi, sheria kandamizi kwa wajane na Watoto wa kike, na ukatili wa kijinsia unaohusihwa na mila potofu.


Pamoja na kutambua na kuchambua changamoto nyingi zilizopo kwenye jamii zao, washiriki walifanikiwa kutoa mapendekezo makuu ya utatuzi kama ifuatavyo:

·       Kuboresha mfumo na utaratibu wa utoaji wa mikopo ya Halmashauri na mafunzo ya uendeshaji miradi/biashara na utunzaji wa fedha kwa wanawake, vijana na makundi mengine ili kupunguza urasimu na kuwezesha upatikanaji rahisi wa taarifa kuhusu fursa kwa makundi hayo.


·       Halmashauri ya Wilaya, hususani, maafisa biashara kwa kushirikiana na sekta binafsi na taasisi zisizo za kiserikali kuwapatia taarifa (kupitia teknolojia ya simu) na kuwajengea uwezo wanawake na makundi mengine ya pembezoni wanaoshiriki katika kilimo kutambua na kufikia masoko na kunufaika na bei nzuri kwa mazao yao.


·       Wajumbe wa Kamati za Vijiji kuweka hamasa na kutumia fursa mbalimbali za kujiongezea uwezo na uelewa kuhusu elimu ya afya ya uzazi ili kuwa mstari wa mbale katika kusimamia kwa ufanisi wa utoaji huduma hizo.


·       Serikali za Vijiji kwa kupitia Utaratibu uliowekwa na TAMISEMI wa Fursa na Vikwazo vya Maendeleo (yaani O&0D) kutambua na kuweka kuwa kipaumbele upatikanaji wa vifaa tiba na idadi ya kutosha ya watoa huduma kwenye zahanati na vituo vya afya.


·       Kuchagiza mapitio na marekebisho ya sheria (Uchaguzi Serikali za Mitaa) na Kanuni ili kuweka mazingira wezeshi kwa wanawake na makundi mengine kujumuishwa na kushiriki kikamilifu kugombea nafasi za uongozi  na vyombo va maamuzi katika ngazi mbalimbali.


·       Kuhamasisha vikundi vya kijamii (wanawake, wanaume, vijana, wazee, watu wenye ulemavu) na Viongozi wa mila na dini ili kuwa mstari wa mbele kutoa elimu na kuongeza uelewa kwenye jamii kuhusu haki za wajane kurithi na kukemea ukatili na dhuluma za ndoa za utotoni na ukeketaji.


Katika siku ya tatu ya Tamasha, washiriki waliandaa mikakati ya utekekelezaji wa mapendekezo yaliyoibuliwa kutoka kwenye warsha kwa kuzingatia hali halisi kwenye kanda, rasilimali zinazowazunguka na kwa kupitia nguvu za pamoja. Kwa namna ya kipekee, mikakati hiyo imetambua umuhimu wa kushirikiana na viongozi wa mila, dini na wa Serikali katika ngazi ya vijiji, kata na Halmashauri.


Katika namna iliyozidi kuheshimisha TGNP kwa kuungwa mkono na Serikali, Mkuu wa Wilaya ya Same, Mheshimiwa Edward Mpogolo atafunga Tamasha la Jinsia ya Kanda akiwa kama mwenyeji wa shughuli zote zilifanyika kwa siku tatu.

Taarifa hii imeandaliwa na:

Idara ya Habari,

Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP
Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post