RAIS SAMIA AONESHA UONGOZI WENYE SURA YA BINADAMU

 

* Viongozi wa upinzani, vyama vya wafanyakazi wampongeza Rais

* Ni kwa uamuzi wake wa kuruhusu zaidi ya watumishi wa zamani wa umma 14,000 waliofutwa kazi kwa kughushi vyeti walipe mafao yao ya pensheni

Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

RAIS Samia Suluhu Hassan amepongezwa kwa uamuzi wake wa kuruhusu watumishi wa umma wa zamani walioghushi vyeti vyao walipwe mafao yao waliyochangia kwenye mifuko ya pensheni.

Wadau mbalimbali wamesema kuwa Rais Samia ameonesha uongozi wenye sura ya binadamu.

"Na hawa bado watasema hawamwelewi Mama (Rais Samia)? Yule kijana sijui kaishia wapi! Kiongozi ni ubinadamu. Mama unao mpaka na chenji inabaki!," Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye, alisema kwenye ukurasa wake wa Twitter.

Naye aliyekuwa Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi, maarufu kama 'Sugu' ameonyesha kufurahishwa na hatua ya Rais Samia kuridhia watumishi wote walioondolewa kazini kutokana na suala la kughushi vyeti kurejeshewa michango yao waliyokatwa kwenye mishahara na kuwasilishwa kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii.

"Hii imekaa vizuri sana Mheshimiwa Rais ⁦Samia⁩ Suluhu Hassan. Ikupendeza walipwe na stahiki zao zingine kama zipo. Maridhiano ni pamoja na kufuta machozi ya wahanga mabalimbali walioathirika kwa namna mbalimbali," Sugu alisema kupitia ukurasa wake wa Twitter.

Viongozi wa vyama vya wafanyakazi nchini nao wamempongeza Rais Samia kwa uamuzi wake wa kiungwana na kuonesha uongozi wenye sura ya binadamu.

"Nimepokea taarifa njema siku ya leo kutoka kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira, Vijana na wenye Ulemavu, Joyce Ndalichako ametutaarifu kwamba Rais Samia ameridhia maombi yetu sisi viongozi angalau kuwalipa wale wafanyakazi waliopata shida ya vyeti," alisema Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Nchini (TUCTA), Tumaini Nyamhokya.

 "Walitoka ghafla hawakulipwa chochote, kiukweli wameumia pakubwa sana, sisi kama wanafamilia wa hao ndugu, tumehangaika kwa namna moja au nyingine kuwasaidia lakini kama viongozi wa vyama vya wafanyakazi tumehangaika sana kuwasemea tangu tulipoingia madarakani mwaka 2016 tukakutana na hiyo dhahama," alisema.

Nyamhokya amesema watu wengi waliathirika na uamuzi ambao ulikuwa umechukuliwa awali lakini kwa kuwarejeshea michango waliyochangia imekuwa faraja.

Elizabeth Kalinga ambaye ni mmoja wa waathirika, amesema wakati anakumbwa na mkasa huo alikuwa Mtendaji wa Kata Iwambi kwa zaidi ya miaka 15 na wakati anapokea taarifa ya kusitishwa kazi alikuwa anaumwa.

"Wakati nakumbwa na hili nilikuwa nimeomba kustaafu maana umri ulikuwa unafika, mwezi wa pili niliomba na mwezi wa tatu nikakubaliwa na mchakato wote ulikamilika na fedha ziliingia lakini nilipozifuata nikaambiwa zimezuiliwa," amesema Elizabeth.

Kwa upande wake, Erasto Mwakapoma aliyekuwa Mtendaji wa Kata ya Ilomba anawashukuru viongozi namna walivyowapigania kwa muda wote.

"Ninamshukuru Rais kwa huruma aliyoiona juu ya yaliyotukuta maana wapo wenzetu waliopoteza maisha, vilema na wagonjwa lakini hatimaye neema imekuja kuonekana kwenye miaka hii angalau tupate kifuta jasho kwakweli namshukuru sana," amesema Mwakapoma.

Rais Samia alitangaza uamuzi wa kuridhia  watumishi wa umma waliondolewa kazini kwa sababu ya vyeti feki, walipwe michango yao waliyochangia kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii, jijini Dodoma na kurushwa mubashara na Televisheni ya Taifa (TBC)  Oktoba 26, 2022.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Joyce Ndalichako amesema utekelezaji wa kurejesha mafao hayo utaanza rasmi Novemba Mosi, 2022.

Watumishi hao ni wale walioondolewa katika utumishi wa umma katika zoezi maalum la uhakiki wa vyeti lililoendeshwa na Serikali ya Awamu ya 5 kwa kushirikiana na Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA) katika kipindi cha kuanzia Oktoba 2016 hadi Aprili mwaka 2017.

Kufuatia uhakiki huo, watumishi wasiopungua 14,516 walibainika kuwa na vyeti vya kughushi na walifukuzwa kazi katika utumishi wa umma.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post