WANANCHI WATAHADHARISHWA DHIDI YA UWEPO WA SURUA

Waziri wa Afya nchini Ummy Mwalimu akizungumza na Waandishi wa habari leo Jijini Dodoma kuhusu kuibuka Kwa ugonjwa wa Surua


Na Dotto Kwilasa,DODOMA.


KUTOKANA na kuwepo kwa ongezeko la watu wenye dalili za homa na vipele vinavyohisiwa kuwa ni ugonjwa wa surua,Serikali kupitia Wizara ya afya nchini imesema inafuatilia kwa karibu magonjwa yanayozuilika kwa chanjo ikiwemo Surua na Rubella.

Waziri wa Afya Ummy Mwalimu amesema hayo leo jijini Dodoma wakati akiongea na waandishi wa habari kuhusu kuwepo kwa ongezeko la wagonjwa wa Surua nchini na kueleza kuwa wahisiwa hao walichukuliwa sampuli na kupelekwa maabara ya taifa ya afya ya jamii kwa ajili ya uchunguzi.

Amesema,uchambuzi wa majibu ya vipimo kutoka maabara hiyo kwa sampuli za kipindi cha Julai hadi Agosti umeonesha kuwa halmashauri saba zimekidhi vigezo vya kuwa na mlipuko wa ugonjwa wa Surua ambapo wagonjwa 38 walithibitika katika Halmashauri za Bukoba (3),Handeni DC(4),Kilindi (3),Mkuranga(4)na Manispaa ya Kigamboni (8).

Nyingine ni Manispaa ya Temeke sampuli (12),Manisapaa ya Ilala Sampuli (4) huku akieleza kuwa  mlipuko wa ugonjwa huo huthibitika pale ambapo sampuli tano za wahisiwa huchukuliwa kutoka katika Wilaya moja ndani ya mwezi mmoja na kwamba endapo sampuli  tatu au zaidi kati ya tano zilizochukuliwa zimetoa majibu chanya.

Pamoja na hayo Waziri huyo wa Afya pia ameeleza kuwa kulingana na uchambuzi huo kulionyesha uwepo wa ugonjwa wa Surua katika Halmashauri za Arusha (1),Chalinze (2),Igunga(1),Kahama MC(1),Kalambo(1),Kigoma DC(2),Kwimba DC(1),Masasi TC(1),Mvomero DC (2),Rorya DC(2) na Manispaa ya Ubungo (2)huku alifafanua kuwa Halmashauri hizi hazikukidhi vigezo vya kuwa na mlipuko wa ugonjwa huo.

Amesema hadi sasa idadi ya wagonjwa wote waliothibitika kuwa na maambukizi ya Surua imefikia 54 kwa kipindi cha Julai hadi Agosti 22 nchini na kufafanua kuwa hadi sasa hakuna kifo chochote kilichoripotiwa .

Sambamba na hayo ameeleza kuwa kati ya wagonjwa 54 waliothibitika kuwa na Surua, wagonjwa 48 walikuwa na umri usiozidi miaka 15 na wagonjwa 6 walikuwa na umri wa zaidi ya miaka 15.

Waziri Ummy pia ameeleza hatua za kuuthibiti ugonjwa huo kuwa ni pamoja na  kuimarisha ufuatiliaji wa wahisiwa kupitia mfumo wa ufuatiliaji wa magonjwa na tetesi katika ngazi ya jamii,kutuma timu kwenda maeneo yaliyo athirika zaidi pamoja na kutoa elimu kwa watoa huduma za afya na jamii kwa ujumla kuhusu dalili na jinsi ya kujikinga na ugonjwa huo

Kutokana na hayo waziri Ummy ametumia nafasi hiyo kutoa rai kwa jamii kupeleka watoto kwenye vituo vya kutolea huduma za afya ili wapatiwe chanjo ya Surua kulingana na umri wao kila wanapofikisha umri wa miezi 9 kwa dozi ya kwanza na miezi 18 kwa dozi ya pili ili kupata kinga kamili.


Kwa upande wake Mkurugenzi wa huduma za Kinga ,Wizara ya afya Dkt.Beatrice Mutayoba alieleza dalili za ugonjwa wa surua kuwa ni pamoja na homa ya vipele inayoweza kuambatana na kikohozi ,mafua,macho kuwa mekundu na vidonda mdomoni na kuelezea kuwa ugonjwa huo hauna tiba maalumu bali matibabu hutolewa kulingana na dalili zilizojitokeza.

Dkt.Mutayoba pia amefafanua kuwa ugonjwa huo usipothibitiwa mapema huleta madhara katika masikio na wakati mwingine hupelekea homa ya mapafu ,upofu wa macho ,homa ya uti wa mgongo na kupoteza maisha.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post